Na: Merinyo
Alhamisi ya tarehe 8 Novemba mwaka huu ilikuwa sikukuu ya wajinga wa Dar es Salaam. Siku hiyo mjinga mmoja au kundi la wajinga lilitunga uzi wa ujinga kwa njia ya uvumi kuwa kuna watu wawili, mwanaume na mwanamke waliokumbwa na dhahama ya kung’ang’aniana katika tendo la uzinzi.
Katika kuendeleza ufumaji wa uzi huo katika tambara jinga la jamii, wazushi hao wakazidi kutia darzi za kila aina, ikiwemo kuwa wawili hao walikuwa wakifanya ngono kinyume na maumbile, wamepelekwa hospitali ya wilaya ya Temeke, wamehamishiwa Muhimbili na kadhalika; alimradi tambara la ujinga la jamii ya Watanzania hususan wa Dar es Salaam lilijaa darizi ya uzushi huo, ukastawi na kuchipua matawi hadi mikoani!
Cha kuhuzunisha na kushangaza katika hili ni kwamba ujinga huu ulitiliwa mbolea, kurutubishwa na kusambazwa na vyombo vya habari na mitandao pendwa ya kijamii ya hapa Tanzania! Maambukizi yakawa si haba, gumzo likanoga maeneo ya kazi, kwenye magari, vijiweni na katika maglobu ya jamii.
Baadaye alasiri vyombo vya habari makini vikaanza kukanusha habari hizo; lakini hadi kesho yake Ijumaa bado kulikuwa na ushabiki mkubwa na hamasa katika sehemu kubwa ya jamii yetu kuhusiana na uzushi huu.
Nimetafakari na kujiuliza: hivi ungetungwa uzushi kuwa kuna kijana kafanya uvumbuzi wa kisayansi na amefaulu kutengeneza kituo chake cha televisheni huko Buguruni na anarusha matangazo bila kizuizi kwa kutumia masafa yasiyoweza kudhibitiwa na Mamlaka ya Mawasiliano; je uzushi huu ungekuwa na hamasa kama hiyo ya ‘fumanizi la ving’ang’anizi vya ngono’?
Jibu nililopata ni hapana! Lakini tukio hili ambalo limetisha kwa mguso na athari zake katika jamii yetu ni mwendelezo tu wa matukio kadhaa yanayoendelea kutokea ambayo yanaelezea undani wa jamii yetu.
Katika mlolongo wa matukio hayo ni pamoja na vurugu za Magala baada ya tukio la kikojozi wa msahafu, maandamano ya Kariakoo ya siku za Ijumaa ambayo yamenisukuma wakati mwingine niite Ijumaa ‘siku ya maandamano’ na yale ya Zanzibar ya siku kadhaa zilizopita.
Matukio haya yote yametudhihirishia jambo moja: kuna wajinga wachache (ambao wanajidhania wajanja!) wamegundua kuwa katika jamii yetu kuna wajinga wengi zaidi ambao wanaweza kulishwa ujinga na wakafanya matakwa ya hao wajinga wachache.
Hawa wajinga wachache wanajua kwamba kuna kundi kubwa la watu, hususan vijana ambao hawana ajira wala kazi ya kudumu, ambao wanaweza kuchukuliwa na uzushi au uchochezi kidogo tu kama vumbi jepesi la kiangazi linavyoweza kutibuliwa na kimbunga na kupaishwa angani, na wakafanya vurugu, maandamano au mwendo-mkumbo mwingine.
Alimradi ibilisi kapata karakana lukuki za kufanyia vitimbi vyake: akili tupu na mikono mivivu. Hapa ninakumbushia hekima zifuatazo: “mikono mivivu ni zana za ibilisi” au “akili vivu ni karakana ya shetani” au “shetani akimkuta mvivu atampa kazi ya kufanya”.
Tumeshaonywa mara nyingi juu ya ukosefu wa ajira kwa vijana katika jamii yetu, jambo ambalo wanasiasa wengi wanalifurahia kwa kuwa linawapa karata ya kutafuta uhalali wa kuwepo. Lakini pia wengi tumefunzwa na tunawafunza watoto wetu kuthamini kazi na kufanya kazi kwani asiyefanya kazi “hastahili kula”, waliyanena wahenga.
Milipuko hii ya maandamano, vurugu na mwendo-mkumbo wa wanajamii ni matunda ya jamii ambayo watu wake wamekubali kuendekeza utamaduni hasi wa ujinga na uvivu.
Hatuwajengei vijana wetu tabia ya kujifunza na kufanya mambo ya kimaendeleo. Ni mara ngapi wazazi wanakaa na kujadili na vijana wao kuhusu mustakbali wao kama familia? Wazazi wengi wameamua kuwaacha watoto wao vijana waishi maisha ya ujanja wa mtaani; na wanashukuru wakiona vijana wao wakiwa wapo wapo tu, wakiamini kuwa watajiweka sawa wenyewe.
Ni mikakati gani inayofanywa na viongozi katika ngazi mbalimbali za kijamii na kiserikali kubuni na kujaribisha mikakati kwa ajili ya kunusuru hali ya vijana kukosa kazi na kuwa zana na karakana ya ibilisi?
Kama jamii tunaendeleza na kujenga mfumo wa fikra na mawazo unaowajenga vijana kuwa wafikirifu na wabunifu au tunaendekeza mifumo hasi ya kifikra kama ile yenye lumbesa ya kingonongono na mawazo yasiyo na tija katika ustawi wetu kama jamii?
Nahofia, tena kwa usahihi kabisa, kwamba kituko cha uzushi cha ‘fumanizi la ving’ang’anizi wa ngono’ limekuja kutudhihirishia pasipo shaka kuwa jamii yetu imefumaniwa iking’ang’aniana na ujinga.
Hofu yangu kubwa kufuatana na tafrani iliyozushwa na uzushi huu ni kwamba huenda kazi ya kuitenganisha jamii yetu na ujinga ni IMPOSSIBLE, au haiwezekani.
No comments:
Post a Comment