Na: Ramadhan Ali na Mwanaisha Mohamed-Maelezo Zanzibar 09/11/2012
Mkurugenzi wa Sauti za Busara ZanzibarYussuf Mahmoud amesema kutokana na malalamiko yanayotolewa na familia ya Bi Fatma Baraka Khamisi (Bi Kidude) wameamua kuzikabidhi fedha za msanii huyo mkongwe alizokuwa akizihifadhi ili kuepusha migogoro zaidi.
Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo huko Kikwajuni wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kufuatia malamiko ya baadhi ya wanafamilia wa Bi Kidude wanaodai kwamba mzazi wao anaibiwa fedha zake na viongozi wa Sauti za Busara.
Mkurugenzi huyo amesema lengo la Sauti za Busara ni kuwasaidia wasanii wa Zanzibar na Afrika kwa jumla katika kuwatangaza na kuwatafutia maslahi ndani na nje ya nchi na sio kuwadhulumu kipato chao.
Amesema baada ya juhudi kubwa walizofanya kuanzia mwaka 2005 walipoanza kumsaidia Bi Kidude ikiwa ni pamoja na kumuwezesha kupata tunzo ya Womex, wamefanikiwa kukusanya shilingi milioni 36 zilizotokana na maonyesho mbali mbali yaliyosimamiwa na Sauti za busara, mauzo ya CD na mahojiano aliyofanya na vyombo vya Habari.
Ameongeza kuwa fedha hizo amekuwa akizutumia mwenyewe, kusimamia kuitengeneza nyumba yake na wamekuwa wakizitumia kwa matibabu yake anapoumwa na hivi sasa fedha zilizobakia ni shilling Millioni tatu laki sita na elfu nne (3,604,000) ambazo zimo mikononi mwake na hivyo alitaka fedha hizo azikabidhi kwa mtu wa familia ambae Bi Kidude ataridhia mwenyewe.
Hata hivyo shughuli ya kukabidhi fedha hizo kwa wanafamilia ilishindikana kutokana na wanafamilia kukataa kuhudhuria katika kikao hicho cha leo.
Mkuu wa miradi wa Sauti za Busara Janny Ramadhani amedai kuwa chanzo cha mzozo ni pale Bi Kidude alipomtambulisha mwanafamilia Baraka Abdalla kuwa ndie atakuwa dhamana wa kumchukulia fedha za kila wiki shilingi 50,000 ambazo walikubaliana lakini baadhi ya wiki kijana huyo alikuwa hazipeleki kwa Bi Kidude.
Amesema familia ya Bi Kidude imechangia kwa kiasi kikubwa katika kumuangusha mzazi wao licha ya juhudi walizokuwa wakizichukua katika kumtangaza na kumpatia safari za mara kwa mara nje na ndani ya nchi.
Viongozi hao wa Sauti za Busra wamewataka wasanii wote nchini wawe pamoja na kujenga moyo wa kushirikiana na kusaidiana ili waweze kukuza vipaji vyao na kuinua sanaa zao na kufikia maendeleo waliyokusudia.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 9/11/2011
No comments:
Post a Comment