Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 9/10/2012
Jumla
ya wanafunzi 800 wa Zanzibar, watafaidika na ufadhili wa masomo ya
Elimu ya Juu Kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzíbar kwa
mwaka wa masomo 2012-2013
Katika Mkopo huo wanafunzi 758 watakuwa wanasomea masomo ya Shahada ya
kwanza, wanafunzi 40 Shahada ya Pili na Wanafunzi wawili wa masomo ya
Shahada ya Tatu kutoka katika vyuo vilivyopo nchini Tanziania.
Akitoa ufafanuzi huo leo Ofisini kwake Shangani Mjini Zanzibar
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Kombo Hassan Juma amesema idadi hiyo ni ongezeko
kubwa kulinganisha na mwaka jana ambapo Jumla ya wanafuzi 209 ndiyo
waliopata Mkopo kutoka kwa Bodi hiyo.
Kombo amesema ongezeko hilo linatokana na kiwango cha Fedha
kilichotengwa na Bodi hiyo kuongezeka ikilinganishwa na mwaka jana
ambapo Jumla ya Shl. Bilioni 8 zitatumika mwaka huu kwa ajili ya
wanafunzi hao.
Amesema kiwango cha mwaka jana ilikuwa Shl.Bilioni 4 ambapo kwa mwaka
huu kimepanda hadi kufikia Asilimia 100 na kufanya mwaka huu Shl.Bilioni
8 kutumika kwa kazi hiyo.
Akielezea maombi yaliyotumwa na wanafunzi waliotaka kupatiwa Mkopo huo
amesema walipokea fomu za wanafunzi 3,500 na hivyo kuwalazimu kuchunguza
wenye vigezo stahiki ambapo waliamua kuwapatia wanafunzi hao 800
kulingana na kiwango cha fedha kilichopo.
Aidha amefahamisha kuwa fani za masomo ya Sheria, Uongozi wa Umma na
Uwalimu wa masomo ya Dini na Kiarabu ni masomo ambayo hayakupewa
kipaumbele katika utolewaji wa Mikopo hiyo.
Amesema Bodi imetoa vipaumbele vyake kwa wanafuzi hao kulingana na
mahitaji ya Serikali ambapo fani za Masomo ya Sayansi na Watu wenye
mahitaji maalumu ikiwemo Walemavu zimepewa umuhimu mkubwa.
Alisema Walemavu wanne ni miongoni mwa watakaonufaika na Mkopo huo kati
yao walemavu wawili ni wenye ulemavu waviungo na wawili Akili
Kwa upende wake Mkurugenzi wa Bodi hiyo Idd Khamis Haji amesema Serikali
inafanya Juhudi za kuhakikisha Vijana wenye sifa wanaendelea na
kujiunga na masomo ya Elimu ya Juu kwa kadiri ya uwezo wa Fedha
utakavyoruhusu.
Aidha Idd amefahamisha njia za kufanikisha lengo kuwa ni pamoja na
Walionufaika na Mikopo hiyo kuhakikisha wanarejesha Fedha hizo kwa
wakati ili kutoa fursa kwa wengine kupata huduma hiyo.
Njia nyingine ni pamoja na kuandaa Matembezi ya hisani, Chakula maalumu
na kuomba misaada kutoka kwa Taasisi za ndani na nje ya Nchi ili
kuhakikisha kila Mwanafunzi wa Zanzíbar mwenye sifa anafaidika na Mkopo
wa Elimu ya Juu.
Idd amewataka Watakaopata mikopo hiyo kwenda katika Ofisi ya Bodi hiyo
ili kuweka Mikataba na kuongeza kuwa majina ya waliochaguliwa kupata
Mkopo huo yatatangazwa punde kupitia Tovuti ya Bodi hiyo na Vyombo vya
habari nchini.
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzíbar ilianzishwa rasmi Julia 2011 kwa
lengo la kusimamia upatikanaji wa Mikopo kwa wanafunzi wa Zanzíbar
ambapo moja ya changamoto kubwa inayoikabili ni ongezeko kubwa la
Wanafunzi wanaohitaji huduma hiyo ikilinganishwa na kiwango kidogo cha
fedha.
No comments:
Post a Comment