tangazo

Tuesday, July 17, 2012

POLISI WAMUOKOA CHIFU

                                                Chifu merere 11 Wa kabila la masangu

CHIFU Merere II (70) (pichani) wa kabila la Wasangu, ameokolewa na polisi kuzikwa akiwa hai baada ya kutokea tafrani katika msiba wa kijana aliyefahamika kwa jina moja la Frank mkazi wa Kijiji cha Ijumbi, Kata ya Ruiwa, wilayani Mbarali mkoani hapa.
Tukio hilo lilitokea baada ya chifu huyo kutuhumiwa kushirikiana na ndugu wa marehemu kwenda kupiga ramli ya ugonjwa wa kijana huyo kabla ya kifo kwa mganga wa kienyeji ambaye jina lake halikutajwa wa Mbozi mkoani hapa, aliyeagiza kuchinjwa ng’ombe mmoja na kupikwa pombe ya kienyeji debe 12 kwa maelezo kuwa mgonjwa angepona.
Kufuatia agizo hilo la mganga, marehemu aliuza shamba kwa shilingi 450,000 kisha fedha hizo kumkabidhi Chifu Merere II kwa ajili ya tambiko na baadaye ng’ombe alichinjwa, pombe ikapikwa na kuitwa baadhi ya wanandugu mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka.
Mganga alidai kuwa waliomroga mgonjwa wao ni ndugu wa karibu na majirani licha ya kutoweka wazi majina yao.
Sakata la Chifu Merere II kutaka kuzikwa akiwa hai limekuja baada ya Frank kufariki dunia Julai 10, mwaka huu na vijana wa Kijiji cha Ijumbi kutaka maelezo kwa nini marehemu alifariki wakati tayari tambiko lilifanyika na fedha zake kuliwa.
Haikuishia hapo, vijana hao waligoma kuchimba kaburi na kumtaka chifu huyo arudishe fedha vinginevyo atazikwa yeye akiwa hai ili iwe fundisho.
Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Jordan Masweve alipopata taarifa hizo alienda nyumbani kwa chifu na kukuta vijana wamemzonga wakimdai fedha zilizotumika katika tambiko ndipo kiongozi huyo alipomchukua na kwenda kumfungia katika mahabusu ya kijiji.
Wanakijiji walichimba kaburi la Frank baada ya kuombwa hivyo na mtendaji huyo, baada ya kumzika marehemu vijana waling’ang’ania kutaka Chifu Merere azikwe hai ndipo taarifa zilipofika polisi na haraka, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Diwani Athuman alipotuma askari kijijini hapo kwa ajili ya kumwokoa kiongozi huyo wa kimila.
Baada ya mazungumzo marefu, Chifu huyo aliweza kurejesha shilingi 350,000 za shamba lililouzwa na akaahidi kiasi kilichobaki kitapatikana siku chache zijazo ndipo aliachiwa huru saa 12 jioni.
Mwanamke mmoja wa Kijiji cha Malamba kata hiyohiyo, Rozina Mwadala(60), alizikwa akiwa hai Juni 2, mwaka huu baada ya mganga huyohuyo wa kienyeji kutoka Mbozi kudai ndiye aliyesababisha kifo cha Frank Lingo (25), aliyefariki Juni Mosi mwaka huu kwa kuugua sikio.

No comments:

Translate