tangazo

Friday, July 27, 2012

MRISHO NGASA BADO ANAIPENDA YANGA.


Na Waandishi Wetu
WAKATI ikidaiwa kuwa majaliwa ya kiungo mshambuliaji Mrisho Ngassa kuwa shakani kwenye klabu yake ya Azam, hali ya mambo sasa inaonyesha ni kama filamu, kwani Ngassa ametamka wazi kuwa anaipenda klabu yake ya zamani ya Yanga ambayo imekuwa ikihusishwa kumsajili.
Ngassa ambaye aliifungia Azam bao la ushindi timu yake katika mechi ya nusu fainali Kombe la Kagame dhidi ya Vita Club ya DR Congo, jana kwenye Uwanja wa Taifa, aliwafuata mashabiki wa Yanga na kushangilia pamoja nao kisha baada ya mechi akarejea tena jukwaani hapo na kupewa jezi ya Yanga kisha kuivaa.
Ngassa aliyekuwa mchezaji pekee wa Azam akishangiliwa na mashabiki wa Yanga katika mchezo huo, baada ya mechi hakutoka uwanjani katika njia moja na wenzake badala yake alielekea kwenye lango lililokuwa na mashabiki wa Yanga ambapo ndipo alipopewa jezi hiyo na kuivaa.
Wakati huo wachezaji wenzake wa Azam FC tayari walikuwa wamerejea vyumbani huku wakisherekea. Baadaye Ngassa aliungana nao akiwa na jezi hiyo ya Yanga aliyoivaa juu ya jezi ya Azam.
“Naipenda Yanga kwa kuwa nimetoka nayo mbali, natamani kurudi ila naheshimu mkataba nilionao kwenye Azam, bao nililofunga limerejesha heshima yangu iliyopotea muda mrefu, kuna mengi yanayoendelea lakini huu siyo muda wake wa kuyazungumza,” alisema Ngassa.
Kumekuwa na taarifa kuwa Ngassa hana uhusiano mzuri na kocha wake katika klabu ya Azam, Stewart Hall na ndiyo maana amekuwa hampangi licha ya kuwa bado yupo kwenye kiwango cha juu.
Alipoulizwa juu ya hilo Hall alisema: “Ngassa ni mchezaji mzuri lakini anahitaji kujituma zaidi ili endelee kucheza kwenye kikosi cha kwanza.”
Mara kadhaa, Ngassa amekuwa akionekana makao makuu ya Yanga mitaa ya Jangwani na Twiga na ilielezwa ilichukua miezi kadhaa kabla ya kurejesha funguo za chumba alichokuwa akikitumia wakati akiwa Yanga.
Ngassa alijiunga na Azam FC kwa kitita cha Sh milioni 98 akitokea Yanga, hata hivyo ameshindwa kuonyesha cheche zake.

No comments:

Translate