tangazo

Tuesday, July 10, 2012

ZIFF YAANZA KWA KISHINDO ZANZIBAR

TAMASHA la Majahazi, ZIFF linalofanyika kila mwaka limeanza juzi kwa staili ya aina yake kwa mashindano ya Ngalawa kutoka Forodhani mpaka fukwe za Chukwani visiwani Zanzibar.

Ngalawa hizo zilipewa majina ya baadhi ya kampuni zinazodhamini tamasha hilo na Zanlink wanaotoa huduma ya mtandao ndiyo waliibuka washindi na kunyakua kiasi cha Sh 200,000.

Mshindi wa pili ilikuwa ni kampuni ya Zat iliyopata Sh 150,000 na Mtoni Marine ilishika nafasi ya tatu na kupata kiasi cha Sh 100,000.

Akizindua tamasha hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Ikaweba Bunting alisema tamasha la mwaka huu kama yaliyopita limemejikita katika kuleta burudani, kuwaunganisha watu wa tamaduni mbalimbali, kutoa ajira kwa Watanzania hasa vijana na kuchangia katika pato la taifa.

“ZIFF ni kiungo muhimu katika kubadilishana utamaduni, kuanzia leo watu kutoka nchi mbalimbali wanakutana, tunaleta siku tisa za kubadilishana utamaduni na kujifunza, Watanzania itumieni fursa hii kujifunza na pia kuonyesha taswira nzuri ya taifa letu,” alisema Bunting na kuongeza;

“Tunaomba muendelee kutuunga mkono kwa kuwa kila mwaka wakati wa tamasha tunaajiri vijana wapatao mia nne, haya ni mafanikio makubwa kwetu na kwa taifa kwa ujumla,” alisema Bunting.

Tamasha la ZIFF litaendelea kwa siku tisa mpaka Julai 15, ambapo mbali na kuonyesha filamu pia litakuwa likisindikizwa na burudani za muziki kutoka kwa wanamuziki nyota wa ndani na nje ya Tanzania.

Nyota watakaolipamba tamasha mwaka huu ni pamoja Jose Chameleone (Uganda), Diamond, Linah, Barnaba, Roma, THT, Dossar, Tausi Women Group,Tazneem.

Upande wa filamu mwigizaji kutoka Marekani, Mario Van Peebles atakuwa mgeni mashuhuri wa mwaka huu na anatarajiwa kuzindua filamu yake, 'We The Party' katika ukumbi wa Cinema Century uliopo mlimani City jijini Dar es Salaam.

Wasanii wa filamu watakaohudhuria ni pamoja na Irene Uwoya, Jackline Wolper, Issa Musa, Jacob Steven, Steve Nyerere na wengine wengi.

No comments:

Translate