tangazo

Friday, July 20, 2012

IDADI YA MAITI WA AJALI YA MV SKAGIT YAFIKIA 62.

                      Baadhi ya maiti zikiwa katika viwanja vya maisara unguja
 
 
SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

WIZARA YA HABARI UTAMADUNI UTALII NA MICHEZO

Tel: 0255 24 2237325/0255 24 223 7313
Maelezo
Fax: 0255 24 2237314
E-mail:habarimaelezo@yahoo.co.uk, maelezozanzibar@zanlink.com
maelezozanzibar@hotmail.com, maelezozanzibar@gmail.com

TAARIFA YA SMZ KUHUSU AJALI YA MELI YA MV. SKAGIT ILIYOTOLEWA
USIKU HUU JULAI 19,2012

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa taarifa usiku wa jana ikieleza idadi ya watu waliopatikana wakiwa hai ni 146 na kupata maiti 62.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari usiku wa jana,Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
Ali Juma Shamuhuna alisema taarifa hiyo ndio sahihi na kuwataka wananchi kutoamini taarifa zinazotolewa na watu wengine zaidi ya Serikali.

Waziri Shamuhuna alisema kwamba maiti 62 walipatikana ambao kati ya maiti hizo watoto ni 9 na kuna raia mmoja wa kike wa kigeni ambaye hakuweza kutambulika Uraia wake,lakini imeonekana picha yake moja ndogo ya hati ya kusafiria.

Waziri Shamuhuna alisema meli hiyo ilibeba jumla ya abiria 290 kati ya hao watu wazima 250,
watoto wadogo 31 na mabaharia 9.

Waziri huyo aliwataka wananchi katika sehemu mbalimbali hasa katika vijiji vilivyo
kandokando ya bahari watakapoona maiti au mtu akiwa hai ambaye wanadhani ni wa ajali ya Meli ya Mv Skagit.

Aidha, Waziri Shamuhuna alisema kwamba kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambao watakuwa na wasiwasi wa kutowaona ndugu na jamaa zao amewataka kufika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kupata taarifa zaidi au kuripoti habari za kupotelewa kwa ndugu au jamaa zao.

Kwa upande wa Zanzibar, Waziri huyo aliwataka wananchi kufika kwa Masheha wao kutoa taarifa kama hizo.

Serikali imewashukuru makampuni binafsi za usafiri baharini kwa msaada wao na wasisite kutoa msaada katika kazi inayoendelea ya kutafuta watu au maiti wengine katika eneo la tukio.

Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 karibu na Kisiwa cha Chumbe umbali wa maili sita
kuelekea Kusini mwa Kisiwa kidogo cha Yasin Zanzibar ikitokea Bandari ya Dar es Salaam ilikoanza safari saa 5:30 asubuhi.

Meli hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Seagul Sea Transport Ltd, Kampuni ambayo Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilizama ikiwa Bandarini Malindi Zanzibar na kufariki watu sita mwaka 2009.

IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
ZANZIBAR, TANZANIA
JULAI 19,2012

No comments:

Translate