tangazo

Tuesday, July 10, 2012

Siku wasomi wa UDSM walivyochambua kazi za Profesa Goran Hyden




ELIMU na  ujuzi havirithishwi kibahati nasibu, bali katika mfumo uliopangiliwa na ndiyo maana hujongea kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Hivi karibuni, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliandaa kongamano la kitaaluma la kuutambua mchango wa Profesa Goran Hyden  katika tasnia ya taaluma Tanzania.

 Profesa huyu  aliyeanza kazi katika  chuo hicho mwaka 1964, amefundisha watu wengi wakiwamo wanasiasa na  wasomi  maarufu hapa nchini. Miongoni mwa  wanafunzi hao ni Rais wa Awamu ya Tatu,  Benjamin William Mkapa.

Tanzania haina budi kujivunia kupewa elimu na Profesa Hyden,  kwani anatajwa kuwa miongoni mwa wanazuoni 20 duniani ambao kazi zao zinasomwa zaidi.

 Kongamano hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam lilihudhuriwa na Waziri Mkuu mstaafu wa Uganda, Apollo Nsibambi  ambaye naye ni mmoja wa wanafunzi wa Profesa Hyden.

Ili kumuenzi Profesa huyo, wasomi walichambua kazi zake,  zikajadiliwa kwa kina, akaulizwa maswali na kisha kutafutiwa suluhisho katika muktadha wa dunia ya sasa.

Mhadhiri  mwandamizi katika chuo hicho,  Profesa Benadeta Kilian, alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani na kuchambua kitabu cha Profesa Hyden kiitwacho,  ‘Beyond Ujamaa in Tanzania: Underdevelopment and Uncaptured Peasant’,  kilichohusu kilimo na ujamaa.

 Profesa Kilian, ambaye naye ni  mwanafunzi wa Profesa Hyden alikichambua kitabu hicho kwa kuainisha ubora wake na maeneo ya upungufu aliyoyaona.

Kwa mfano, alisema:   “Kitabu kile kiligusa zaidi mfumo wa chama kimoja wa wakati ule. Hivyo basi ipo haja ya kubadilisha baadhi ya mambo yaliyokuwepo katika kitabu ili kiendane na muktadha wa sasa,”

 Akiendelea kukichambua kitabu hicho, Profesa Kilian akizungumzia dhima kuu ya kitabu hicho ambayo ni  kilimo, anasema iko haja ya kumuangalia mkulima zaidi ili kuleta maendeleo Tanzania.

“Sera ya kilimo kwanza si mbaya, ila tuna nafasi ya kuiboresha ili kufanikisha azma hiyo, “anasema na kuongeza kuwa badala ya kuiita sera hiyo kilimo kwanza, ni vema  ikaitwa ‘mkulima kwanza’

“Mkulima amesahauliwa, tukisema tukipe kipaumbele kilimo, tutajikuta tunamsahau mkulima. Kilimo ni dhana pana na ndiyo maana hatuna budi kuivunjavunja,  na tuanze kwa kumuenzi mkulima kwanza,” anafafanua.

 Wanazuoni wengine walikubaliana na Profesa Hyden kuwa, mkulima mdogo Tanzania bado hajaendelezwa na kuwa Mwalimu Julius Nyerere hakutumia njia bora za ‘kumteka’ kimaendeleo mkulima huyo.

Msomi mwingine aliyechambua maudhui ya kitabu hicho ni Profesa Profesa Humphrey Moshi anayesema sera ya kilimo kwanza imekosa mvuto na malengo yake yameyeyuka mithili ya barafu katika moto.

Anasema alipokuwa akifanya utafiti  kuhusu  kilimo na ufugaji wilayani Hanang katika  Mkoa wa Manyara , alijionea namna  matrekta madogo ya kilimo maarufu kwa jina la Power Tiller yakitumika kubeba bidhaa na abiria  badala ya kulima.
“Mipango mibovu ya kilimo kwanza ndiyo inayokwamisha mafanikio ya sera hiyo.

‘Power Tiller’ zilizopelekwa Babati, haziendani na  mazingira ya kilimo cha alizeti
kinachofanywa pale,” anasema.

Kwa upande wake, Profesa Hyden anasema  wakati wa sera za Ujamaa,  Serikali haikutoa njia bora za kumfanya mkulima afanikiwe, ili   aliletee Taifa lake  maendeleo.

Anatoa mfano kuwa Serikali ilitumia njia dhaifu za kumbadili mkulima, hivyo kumfanya aendelea kuukumbatia ujadi.

“Ujamaa ulichochea kufeli kwa wakulima. Waliendeleza uchumi wa kufadhiliana na zaidi hasa waliendelea kuitegemea Serikali katika huduma kuu za kijamii,” anasema.

 Anasema kosa kubwa lilikuwa pale uchumi wa kufadhiliana ulipotumika, kiasi cha  kudunisha shughuli za uzalishaji viwandani na kwa wafanyakazi.

Kwa mfano,  anaeleza kuwa watu waliendelea kupata huduma za afya, maji na elimu bure,  hivyo hawakuona haja ya kuwajibika kwa asilimia 100.

Hata hivyo,   anatoa suluhisho kwa kusema: “Hatuna budi kuwaacha wakulima wakubwa waje kutufunza mbinu za kilimo, ni nafasi muhimu kwa wakulima wadogo kujifunza.”

Dk Benson Bana, aliyekuwa mmoja wa waratibu wa kongamano hilo anasema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kimejiwekea utaratibu wa kutoa nishani za kutambua michango ya wanazuoni muhimu.

“Tunafanya hivi ili kuwapa motisha, hatupendi kuwapa sifa  baada ya kufariki, bali wakiwa hai, ili waishuhudie shukrani tunayowapa,” anasema.

Anaeleza kuwa  mchango wa Profesa Hyden ni  muhimu,  kwani kazi zake nyingi alizoandika zinatumika hadi leo kitaaluma na hata katika uwanja wa maendeleo.

“Profesa Hyden alifanya tafiti nyingi, mojawapo ni  utafiti kuhusu utumiaji wa sera na maendeleo Tanzania, “ anasema Dk Bana

 Anabainisha kuwa  kongamano  hilo mbali ya kumuenzi mwanazuoni huyo,  lakini pia lilikuwa darasa  tosha kwa wasomi wa sasa kwa kuwa  linawafumbua macho kuhusu hatima ya Tanzania na maendeleo yake.

 Wasifu wa Profesa Hyden
Goran Hyden alizaliwa mwaka 1938 nchini Sweden. Anatambulika kama Mwana Afrika na mwanazuoni farisi wa masuala ya Sayansi ya Siasa.

Alipata elimu yake katika vyuo vikuu mbalimbali kama vile,   Chuo Kikuu cha Florida,  Chuo Kikuu cha Lund, Chuo Kikuu cha  Oxford na Los Angeles (UCLA).

Alitumia  muda wake mwingi kufundisha katika vyuo vikuu vya Afrika mashariki , vikiwamo  Chuo Kikuu cha Makerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na  Chuo Kikuu cha  Nairobi.

Profesa Hyden amefanya tafiti mbalimbali zinazohusu uchumi, siasa na maendeleo hasa katika nchi za bara la Afrika. Alistaafu mwaka 2009 akiwa na tuzo zaidi ya 25 alizopata kutokana na ubora wa kazi zake.

No comments:

Translate