tangazo

Tuesday, August 7, 2012

MGOMO WA WALIMU NI SAWA NA TEMBO WAWILI WANAPOPIGANA, ZIUMIAZO NYASI

                                  Rais Chama cha Walimu nchini (CWT) Gratian Mukoba.


TUNAMUOMBA Mungu atuepushie balaa ya mfarakano na atutie nguvu ili tuzidi kushikamana.
NDUGU zangu, wiki  nzima iliyopita nchi imejikuta ikitikisika kutokana na mgomo wa walimu uliotanda  sehemu mbalimbali nchini  wakiishinikiza serikali kuwalipa stahiki zao, huku ukiathiri sekta ya elimu katika ngazi za shule za msingi na sekondari za umma kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na taarifa mbalimbali ukweli ni kwamba katika sehemu nyingi za nchi walimu waligoma kuingia madarasani na wengine walifika tu kazini na kusaini vitabu vya mahudhurio kisha kuondoka. Kama mzazi, hii inauma sana!

Inauma kwa sababu watoto wetu wanakosa elimu na wengine wapo darasa la saba huku wengine wakiwa kidato cha nne au cha sita, wote siku zijazo watafanya mitihani bila kujali kama walikuwa wakifundishwa au la.

Wahenga walisema tembo wawili wapiganapo, ziumiazo nyasi. Ndivyo ilivyo, walimu na serikali wanapogombana watakaoumia ni wanafunzi. Ni wazi wengi watafeli mitihani yao kwani watakuwa nyuma ya silabasi.

Cha ajabu ni kwamba licha ya walimu kugoma, wanafunzi katika baadhi ya shule za msingi walifanya maandamano kupinga hatua hiyo.

Wengi walionekana katika vyombo vya habari wakiandamana na kupiga kelele wakisema mgomo huo ulikuwa unawanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Picha za luninga na magazeti zilionyesha madarasa katika baadhi ya shule yakiwa matupu au yakiwa na wanafunzi lakini bila kuwapo walimu. Picha nyingine zilionyesha wanafunzi wakiwa madarasani wakifundishwa na wenzao waliochukua nafasi za walimu wao.

   Wengi tunajiuliza, nani aliwahamasisha wanafunzi hao kufanya maandamano nchi nzima? Ni swali gumu la kitendawili ambacho huenda itakuwa vigumu kukitegua katika siku zijazo kwani halihitaji majibu mepesi.
Kinachonishangaza mimi bila shaka na Watanzania wengine ni hatua ya jeshi la polisi kumwaga askari wenye silaha za moto barabarani kukabiliana na watoto hao wa shule waliokuwa wakiandamana.

Ilisemwa kuwa walikuwa wakielekea katika ofisi za mamlaka husika kupinga mgomo huo ambao Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema hautakuwa na kikomo.

Tuliona katika magazeti  baadhi ya polisi wakitumia nguvu kupita kiasi kuwakamata wanafunzi hao kama wanavyofanya wanapowakamata majambazi wenye silaha za moto au za kivita.

   Hapa ndugu zangu natoa ushauri wa nini kifanyike licha ya serikali kujiona imeshinda mahakamani dhidi ya walimu, warudi katika meza ya mazungumzo kwa lengo la kupata maridhiano.
Kwanza, niseme wazi kuwa walioishauri serikali kupeleka suala hilo mahakamani hawakutumia busara kwa kuwa lilikuwa bado linazungumzika.

Kusema kweli haitoi picha nzuri hata kidogo kwa serikali kukimbilia mahakamani kila inapoingia katika migogoro na wafanyakazi na haipaswi kuiona mahakama kama kimbilio pekee kila wakati Tume ya Usuluhishi na Uamuzi  inaposhindwa kutatua mgogoro katika muda mfupi.
Sehemu nyingi duniani tumekuwa tukiona kwamba utatuzi wa migogoro unahitaji uvumilivu na subira kubwa kwa pande zinazopatanishwa.

 Msisitizo hapa ni kwamba, mchakato mzima wa kumaliza mgogoro wowote ule unahitaji kuvumiliana, kusikilizana na kuheshimiana. Kwa maana ya kila upande kujaribu kuelewa hoja za mshindani wake.
Lakini pia kila upande katika mgogoro unatakiwa  kutambua na kukubali ukweli kuwa, katika mapatano ya usuluhishi hakuna upande unaoweza kupata kila kitu unachotaka.

 Kwa mfano, katika mgogoro huu ulio mbele yetu, walimu lazima waelewe kwamba hawawezi kuongezewa mshahara kwa asilimia 100 kama wanavyotaka.

Kwa mtu anayefikiri kwa kina na kutafakari mambo, atagundua utamaduni wa serikali kukimbilia mahakamani badala ya kutafuta maridhiano na wafanyakazi ni uthibitisho kwamba sheria za kazi zina mapungufu makubwa.

 Kwa mfano, inakuwaje Kifungu cha 83(4)g cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004 itamke kwamba mwajiri hatalazimika kulipa mshahara kwa mtumishi aliyeshiriki katika mgomo, hata pale ambapo chama cha wafanyakazi kitakuwa kimefuata sheria na taratibu zote za kutangaza mgomo?

   Katika sakata la mgogoro huu serikali imesema mgomo wa walimu uliokuwa ukiendelea ni batili kwa sababu shauri lake lilikuwa mahakamani.

Kwa tafsiri na wasomi na watu wanaotafakari mambo mazito ni kwamba  pengine kitendo cha serikali kukimbilia mahakamani kuzuia wafanyakazi wasitekeleze haki yao ya kugoma baada ya kufuata sheria na taratibu zote zilizowekwa ni matumizi mabaya ya mhimili huo wa dola maana sheria ni msumeno.

Njia pekee ya kumaliza mgogoro ni wizara ya elimu chini ya Waziri Dk. Shukuru Kawambwa kukaa meza moja na CWT chni na kiongozi wao, Gratian Mkoba kujadiliana. Hata watu wanaopigana vita hufanya hivyo, kwa nini serikali na CWT washindwe?   Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Translate