tangazo

Friday, August 3, 2012

SERIKALI ILIFIKIRIE MARA MBILI MWANAHALISI


SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano kupitia msajili wa magazeti ambayo ni Idara ya Habari (Maelezo), imelifungia Gazeti la Mwanahalisi kwa muda usiojulikana.
 

Uamuzi huo, ulitolewa Jumatatu ya wiki hii na Kaimu Mkurugenzi wa Maelezo, Phabian Lugaikamu, akibainisha kwamba serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, inalifungia Mwanahalisi kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za uchozezi.

Lugaikamu alifafanua kwamba Mwanahalisi limekuwa likijenga uhasama na uzushi, likiwa na nia ya kusababisha wananchi wakose imani na vyombo vya dola, hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa nchi.

Akafafanua pia kwamba gazeti hilo namba 302, 303 na 304 ya mwaka 2012 na mengine yaliyotangulia yalichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.

Pamoja na ufafanuzi mzuri wa serikali na hoja zake za kulifungia gazeti hilo, sisi Global Publishers (wachapishaji wa magazeti pendwa nchini, Uwazi, Ijumaa, Amani, Risasi, Ijumaa Wikienda na Championi), tunashauri uamuzi huo ufikiriwe mara mbili.

Ni ukweli kwamba serikali imetumia haki na mamlaka yake kutokana na meno iliyopewa kupitia sheria ya magazeti nchini ya mwaka 1976, kifungu nambari 25 (i), lakini ni rai yetu kuangalia pia athari za upande wa pili baada ya kulifungia gazeti hilo.
 
ATHARI NAMBARI MOJA
Athari ya kwanza ambayo sisi Global tunaiangalia ni kutetereka kwa ajira za wafanyakazi wa Kampuni ya Hali Halisi Publication, inayochapisha gazeti hilo. Mwanahalisi kama uti wa mgongo wa kampuni hiyo, kusimamishwa kwake kunahatarisha ajira za wafanyakazi wake.

Uhai wa kampuni unategemea uzalishaji, sasa kampuni kama haizalishi, ni wazi haitaweza kulipa mishahara wafanyakazi wake. Tunaomba serikali itupie jicho eneo hili.
 
ATHARI NAMBARI MBILI
Sisi Global, tunatambua na kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo basi tunaelewa uwepo wa kifungu namba 30, kinachofafanua juu ya kikomo cha uhuru wa kutoa maoni.

Hata hivyo, ndani ya katiba hiyohiyo, Ibara ya 18, inatoa uhuru wa mtu kutoa maoni. Vema serikali ikarejea Ibara ya 18 kisha kupima mara ya pili na kujiridhisha kuhusu uamuzi wake wa kulifungia gazeti hilo.
 
HITIMISHO LETU
Sisi Global, tunaiheshimu serikali na uamuzi wake iliyochukua dhidi ya gazeti hilo. Hata hivyo, kupitia athari ya kutetereka kwa ajira na kipengele cha kuonekana inaingilia uhuru wa habari na utoaji maoni, tunaishauri kufikiria mara mbili na ikiwezekana, ilisamehe Mwanahalisi liendelee kufanya kazi yake.

No comments:

Translate