tangazo

Wednesday, July 4, 2012

MUNGU MKUBWA, HATIMAE FIGO ZA DR ULIMBOKA ZAANZA KUFANYA KAZI.



AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka imeendelea kuimarika baada ya kupata matibabu nchini Afrika Kusini na sasa figo zake zimeanza kufanya kazi.Dk Ulimboka alipelekwa nchini huko mwishoni mwa wiki baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kiasi cha kusababisha figo zake kushindwa kufanya kazi.Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema Dar es Salaam jana kwamba, hali ya Dk Ulimboka imeimarika na kuwaomba Watanzania wamuombee apone haraka.“Taarifa tulizozipata kutoka Afrika Kusini zinasema kwamba, hali ya Dk Ulimboka imezidi kuimarika tofauti na alivyokwenda, figo zimeanza kufanya kazi ingawa kwa polepole na amefanyiwa vipimo vingine,” alisema Dk Kabangila na kuongeza:

“Pia ameanza kuzungumza, anawatambua watu vizuri na zaidi amewaomba Watanzania wamuombee apone haraka.”
Awali, chanzo kimoja cha habari kilidokeza kwamba hali ya Dk Ulimboka imeimarika kutokana na kupatiwa huduma za matibabu kwa haraka kwa kufanyiwa pamoja na vipimo vingine, kile cha usafishaji damu na figo (Dalysis), mara kwa mara. Kabla ya kuondoka nchini, Dk Ulimboka alifanyiwa usafishaji huo mara mbili.

Madaktari walisema kuwa, kipimo hicho kililenga kupunguza kiwango cha sumu iliyoonekana kwenye damu, ambayo haikutambulika mara moja kama ilitengenezwa ndani ya mwili au vinginevyo kwa kuwa hakuna kipimo cha kubaini tatizo hilo nchini.

Migomo hospitalini
Licha ya huduma kurejea taratibu katika baadhi ya hospitali nchini, mgomo wa madaktari bingwa umeendelea chini kwa chini.Pia jana, Serikali imewataka madaktari wote walio katika mafunzo ya vitendo kuripoti Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ifikapo Ijumaa.

Jana, wizara hiyo ilitoa taarifa ikitaka madaktari wote nchini wanaofanya mafunzo kwa vitendo (interns) ambao walipewa barua za kurudishwa wizarani, kuripoti Dar es Salaam Julai 6, mwaka huu.

Mgomo wa madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), umekuwa na utata baada ya kuwapo taarifa mbili zinazokinzana.

Uongozi wa (MNH) kupitia kwa Msemaji wake, Aminiel Aliegaeshi umetoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari jana ukisema huduma za matibabu zinaendelea kama kawaida, lakini kwa kiwango cha kati.

“Huduma hapa hospitalini zinaendelea kutolewa kwa kiwango cha kati, wagonjwa ni wachache wanaokuja kutibiwa. Madaktari Bingwa wote wameingia na kufanya kazi na Interns kumi na moja wamefanya kazi,” alisema.

Jana waandishi wetu walishuhudia baadhi ya huduma zikiendelea kutolewa kama kawaida katika hospitali hiyo zikiwemo x-ray katika Taasisi ya Mifupa (Moi) na hospitali hiyo kuu.

Awali, huduma hiyo na nyingine zilisimama baada ya tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka.

Lakini, wakati Aliegesha akitoa taarifa hiyo, madaktari bingwa wamesisitiza kuwa wako kwenye mgomo huku msemaji wao, Dk Cathrine Mng’ong’o akitaka waandishi wa habari kulinganisha maneno hayo ya uongozi na hali halisi hospitalini hapo.

“Mimi siwezi kujibu swali hilo (kama wako kwenye mgomo au wamerudi), sababu sipo katika eneo la hospitali leo, niko nyumbani. Wewe angalia kwa macho yako uone kisha linganisha maneno hayo na hali halisi,” alisema Dk Mng’ong’o.Alipoulizwa kuwa kama jana alikuwa zamu alijibu kwa kifupi kuwa madaktari bingwa hawana zamu na hufanya kazi saa 24.

Madaktari hao juzi walitangaza mgomo wakitaka Serikali kuwarudisha kazini madaktari wote waliofukuzwa.

Uongozi wa MNH ulisema, idara ambazo madaktari walikuwapo ni ya huduma za dharura na katika vitengo vingine ilidaiwa kuwa walifika kwa kiwango kikubwa.

Katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, hali imezidi kuwa tete baada ya wagonjwa kuhamishiwa hospitali za binafsi kutokana na kuzorota kwa huduma.Mkazi wa Sakina aliyejitambulisha kwa jina moja la Manka, ambaye mtoto wake alikuwa amelazwa hospitalini hapo akisubiri upasuaji alisema, amelazimika kumhamisha mtoto wake kutokana na kukosa huduma.

Hata hivyo, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Eliringia Mlay alikanusha madai ya kuwapo kwa mgomo hospitalini hapo na kusema kuwa, ulikuwapo awali lakini kwa sasa umekwisha na madaktari wanaendelea na kazi kama kawaida. Hospitali binafsi

Hospitali ya TMJ imeanza kutoa huduma ya tiba kwa baadhi ya wagonjwa waliokuwa Muhimbili baada ya kuingia mkataba na Serikali ili kutoa huduma ya matibabu katika kipindi ambacho madaktari wa Serikali wapo katika mgomo.

Msemaji wa Hospitali hiyo, Huzaifa Seif alisema jana kuwa wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali hiyo ni wale wenye kadi za Bima ya Afya na wagonjwa walioandikiwa rufaa kutoka MNH.
Hata hivyo, mmoja wa wagonjwa, Anaeli Mbasha alisema ingawa Serikali imeingia mkataba na hospitali hiyo, wagonjwa wengine wenye kipato kidogo wanashindwa kuhimili malipo.

Hospitali ya Regency imekuwa na ongezeko la wagonjwa ikiaminika kuwa ni kutokana na mgomo huo wa madaktari. Mmoja wa madaktari hospitalini hapo, Dk Emmanuel Jonathan alisema wagonjwa ni wengi hasa kutoka Muhimbili.

Katika Hospitali ya Aga Khan, baada ya wiki iliyopita kuwa na ongezeko la wagonjwa kwa asilimia 15, idadi hiyo imepungua kati ya jana na juzi.Mkurugenzi wa Tiba wa Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee alisema: “Ongezeko kubwa lilikuwa katika vipimo ambavyo vinapatikana katika Hospitali ya Muhimbili na hapa (Aga Khan), peke yake kwa mfano MRI (Magnetic Resonance Imaging).”

No comments:

Translate