tangazo

Wednesday, July 4, 2012

KESI YA MSANII MARUFU WA FILAMU NCHINI,AMBAE ANATUHUMIWA KWA KESI YA MAUWAJI YAZIDI KUPIGWA TAREHE.


                             Msanii wa filamu nchini Elizabet Michael Akiwa mahakamani.



MSANII maarufu wa filamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ amechimba mkwara mzito katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini Dar es Salaam, Risasi Mchanganyiko linatiririka.
Lulu ambaye ni mshukiwa namba moja wa kifo cha msanii mwenzake, marehemu Steven Kanumba, alichimba mkwara huo, juzi Julai 02, mwaka huu wakati akifikishwa mahakamani hapo, kesi yake inapoendeshwa.


ATEMA CHECHE
Baada ya Lulu kushuka katika gari la Magereza na kusindikizwa kwenda kizimbani na askari Magereza, alianza kumshambulia mwandishi wetu kwa maneno alipomuona amekazana kupata picha zake.
“Hivi hamchoki kunifuatafuata? Kila siku Lulu, Lulu niacheni na maisha yangu! Kwani kuna kitu gani kipya tena?
“Hivi nyie hamna kazi nyingine ya kufanya...baba mzima unahangaika kunifuatilia? Nimechoshwa na tabia yenu bwana,” alibwatuka Lulu bila woga.


ASKARI WAPIGWA NA BUTWAA
Wakati Lulu akitema cheche, askari waliokuwa ‘wakimueskoti’ walibaki wamepigwa na butwaa bila kuamini kama ni kweli Lulu ndiye aliyekuwa akizungumza kwa ujasiri mkubwa kiasi kile.
Mdau mmoja aliyekuwepo mahakamani hapo, alisikika akisema: “Mh! Mwanzoni Lulu alikuwa analia kila siku, lakini sasa naona ameanza kuzoea...amekuwa mbogo huyo!”


KESI YAKE NENDA RUDI
Kesi ya Lulu imeonekana kuwa na mvutano mkubwa huku matumaini ya kuanza kusikilizwa yakionekana kuwa hafifu kutoka na shauri hilo kuendeshwa katika mahakama mbili tofauti.
Awali, Mwendesha Mashitaka wa kesi hiyo, Elizabeth Kaganda, mbele ya Hakimu Agustina Mbando alisoma kesi hiyo lakini kabla ya mtuhumiwa hajajibu chochote, hakimu aliihairisha kesi hiyo.
Hakimu Mbando alisema, analazimika kuhairisha kesi hiyo hadi Julai 16, mwaka huu kwa vile shauri hilo halijakamilika kwa sababu lipo Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam ikijadiliwa suala la umri.
Hata hivyo, mahakama kuu ilipeleka shauri hilo katika mahakama ya rufaa baada ya mawakili upande wa serikali, kupinga suala la umri wa Lulu kujadiliwa mahakamani hapo, badala yake lipelekwe katika mahakama ya rufaa.
Mawakili hao walisema, kwa sasa Lulu atabaki kujulikana kuwa ana umri wa miaka 18, ambao aliandikisha yeye mwenyewe katika Kituo cha Polisi Oysterbay alipokuwa akihojiwa kwa mara ya kwanza baada ya kukamatwa.


NDUGU, WASANII WAMTOSA
Aidha, siku hiyo hakukuwa na ndugu yeyote wa Lulu wakiwemo wazazi wake aliyefika mahakamani hapo kufuatilia shauri hilo.
Ukiachilia mbali hao, hata wasanii wenzake ambao wana jumuiya mbalimbali kama Bongo Movie na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) pia hawakufika kumuona mwenzao.


KUMBUKUMBU MUHIMU
Lulu alikamatwa Aprili 07, mwaka huu kwa madai ya kuhusika na kifo cha marehemu Kanumba, kilichotokea nyumbani kwake, Sinza - Vatican, jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia siku hiyo.
Kwa sasa yupo katika Gereza la Segerea huku kesi yake ikiendelea kuunguruma katika mahakama mbili tofauti; Hakimu Mkazi, Kisutu na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

No comments:

Translate