Maandamano ya kuipinga Japani
yameendelea katika miji kadha ya Uchina katika mzozo unaozidi kuhusu
visiwa vilioko katika bahari ya kusini ya Uchina.
Polisi walitumia gesi kutawanya watu
waliokuwa na hasira kwenye mji wa Shenzhen, kusini mwa Uchina, huku
waandamanaji wakichoma bendera za Japani katika mji wa jirani,
Guangzhou.
Japan imetoa wito kwa Uchina kuhakikisha usalama
wa raia wa Japani, huku Uchina imezidi kusisitiza madai yake ya visiwa
hivo viitwavyo Senkaku au Diaoyu.
Kwa miaka mingi hayakutokea maandamano ya ghasia Uchina kama haya, kuipinga Japani.
Watu waliokuwa na hasira walichoma moto bendera ya Japani, walibeba mabiramu ya kuitusi Japani na kurusha mawe ubalozini.
Karakana na biashara za Japani piya zililengwa na waporaji na kuchomwa moto.
Hata hivo maandamano hayo hayakutajwa na vyombo vya habari vya taifa na juhudi zimefanywa kudhibiti majadiliano kwenye internet.
Sababu ni kuwa maandamano yenyewe ni mazuri kufikisha ujumbe kwa Japani, lakini yanaweza kugeuka na kuwa dhidi ya serikali piya.
Wakuu wa Uchina wanaamini kuwa Japani imevunja makubaliano ya namna fulani, kwamba hali ibaki kama ilivokuwa.
Serikali ya Japani inasema inavinunua visiwa
hivo kutoka serikali ya mji wa Tokyo ili kuzuwia serikali ya jiji
kufanya miradi na kujenga katika visiwa hivyo.
Lakini Uchina inaona hatua hiyo ni juhudi za kuthibitisha kuwa visiwa hivyo ni vya Japani.
No comments:
Post a Comment