Mkwaju wa penalti wa Frank Lampard katika dakika za
mwishomwisho uliiwezesha England kuondoka na angalau pointi moja katika
mechi ya kufuzu kushirikishwa katika michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya
Ukraine, katika uwanja wa Wembley.
Yevgeni Konoplianka aliweza kufunga bao la
kusisimua katika kipindi cha kwanza na kuiwezesha Ukraine kupata nafasi
ya kuongoza, hadi zikiwa zimesalia dakika tatu mechi kumalizika, juhudi
za England hatimaye zilipata ufanisi.
Mchezaji wa zamu Danny Welbeck ambaye
alibadilisha mchezo tangu alipoingia, alishuhudia juhudi zake zikizimwa
kwa njia isiyo halali na Yevgeni Khacheridi, na kutokana na adhabu
iliyotolewa ya penalti, Lampard, kama ilivyo desturi, akiwa makini na
mtulivu, aliweza kufunga bao la kusawazisha.
Baadhi ya wachezaji mahiri wa England hawakuweza
kushiriki katika mechi hiyo, na ilikuwa ni pigo kubwa zaidi baada ya
nahodha Steven Gerrard naye kuamriwa na mwamuzi kuondoka uwanjani, baada
ya kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano, na inamaanisha mchezaji huyo
sasa ataikosa mechi nyingine ya kufuzu katika uwanja wa Wembley mwezi
Oktoba, wakati timu yake itakapopambana na San Marino.
Ilikuwa dhahiri kwamba matokeo hayo
yalimridhisha meneja wa England Roy Hodgson, ambaye ilikuwa wazi uso
wake ulionyesha baada ya timu yake kuwakosa wachezaji mahiri kupitia
maradhi na majeraha, ilikuwa ni afadhali kuondoka na hiyo pointi moja
badala ya kuondoka pasipo lolote, na ilikuwa ni kinyume na Ijumaa
iliyopita wakati walipoinyeshea Moldova magoli 5-0 huko Chisinau.
No comments:
Post a Comment