Polisi na wataalamu wa kuchunguza maiti wamepigwa na
mshangao mkubwa baada ya kukosa kupata chochote ndani ya makaburi ya
siri yaliyogunduliwa katika eneo la Tana River.
Polisi walipewa amri ya kufukua makaburi hayo
hii leo katika kijiji cha Ozhi ambako mapigano kati ya jamii za Orma na
Pokomo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu miamoja na kuwaacha maelfu
bila makao.
Kwa mujibu wa naibu kamishna wa
polisi eneo la Tana River, Anthony Kamitu, makaburi hayo yalikuwa na
mitaro minne ishara kuwa watu walikuwa wamezikwa kwenye makaburi hayo.
Ingawa bwana Kamitu alisema kuwa hawakupata
miili yoyote licha ya kuwa kulikuwepo na harufu mbaya ishara kwamba
maiti waliokuwa ndani ya makaburi hayo waliondolewa.
Bwana Kamitu anasema kuna hofu kuwa wahalifu
kutoka jamii ya Pokomo waliitoa hiyo miili kwenye makaburi hayo huku
polisi wakisubiri kibali cha mahakama ili kuweza kuyafukua.
Polisi wamefahamisha BBC kuwa makaburi hayo
yalikuwa tu na mguu mmoja wa kushoto wa mtu na wanashuku kuwa maiti
waliokuwa ndani ya makaburi hayo waliondolewa na kupelekwa kwingineko.
Zaidi ya watu miamoja wamefariki katika mapigano
kati ya jamii hizi mbili ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda wa mwezi
mmoja ulipita.
Makabiliano kati ya jamii hizo mbili yalianza
katikati ya mwezi jana na kusababisha mashambulizi ya kuvizia na ya
kulipiza kisasi.
No comments:
Post a Comment