tangazo

Tuesday, September 11, 2012

YALIYOJIFICHA KIFO CHA MAREHEMU DAUD MWANGOSI

                           
                                                     Marehemu Daud Mwangosi.

KWA akili ya kawaida mtu anaweza kujiuliza kulikuwa na sababu gani kwa polisi kumfyatulia bomu mwandishi wa habari marehemu Daud Mwangosi kama kweli inavyosemwa ndivyo ilivyo?
 

Sakata la kuuawa kwa Mwangosi lililotokea mjini Iringa hivi karibuni limeonesha udhaifu mkubwa wa kimaamuzi kwa askari waliokuwa eneo la tukio kiasi cha kunifanya nianze kuamini kuwa kuna baadhi ya polisi wamehongwa wavuruge amani  ili wadowezi wa madaraka wapate nafasi ya kuingia Ikulu.
 

Ushahidi wangu juu ya hilo ni namna picha za tukio la mauaji ya kinyama zinavyoonesha polisi zaidi ya tisa wakiwa wamepandisha wazimu kumsulubu mtu ambaye hakuwa na silaha, hakuwa anajihami kwa chochote.
 

Najiuliza: Haikutosha kumpiga mwandishi kwa mateke, kumtandika ngumi na virungu  mpaka ikabidi kumtuliza kwa bomu? Kama si usaliti ndani ya jeshi la polisi ni nini?
 

Nina imani isiyo na shaka kuwa, nyuma ya matukio ya kijinga namna hii kuna mpango wa kuichonganisha serikali na wananchi ili kuleta mapinduzi ya umma.
 

Maana ni wazi wanaotumwa kuchafua hali ya hewa kwa kufanya mambo ya kijinga wanaamini mwisho wa safari jamii haitawalaumu wao bali rais na serikali yake.
 

Mfano, polisi wanaodaiwa kumuua mwandishi wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuamsha hasira za wananchi kwa serikali. Jamii imelishwa sumu kuwa yote yaliyotokea ni mapenzi ya Waziri wa Mambo ya Ndani,
 

Dk. Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema.
Maneno yanayouzwa mitaani kwa mtaji wa mauaji ni “waziri na IGP waachie ngazi.” Sababu za kufanya hivyo, eti wamegeuza majukumu yao kichwa chini miguu juu, yaani wameshindwa kulinda raia na badala yake wanawaua.
 

Nimezoea kupinga kwa hoja:  Hivi IGP aagize polisi wamuue mwandishi wa habari ili iweje? Awatume askari wake wampige risasi muuza magazeti ili anufaike na kitu gani? Waziri awatume polisi kutembeza mijeledi kwa raia ili apate faida gani? Wenye majibu wanaweza kunisaidia kwa lengo la kunielewesha zaidi.
 

Binafsi nabaki kuamini kuwa, Tanzania ya leo ina mawaziri watiifu na waasi, polisi waaminifu na wahalifu, watendaji watiifu na waasi. Huyu ndiye shetani anayeiyumbisha serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na siku si nyingi ataiangusha.
 

Katika hali ya kawaida waasi huwa hawakosekani miongoni mwa jamii kwani hata Yesu Kristo aliyekuwa na wanafunzi 12 mmoja kati yao alikuwepo Yuda anayetajwa kumsaliti.
 

Kwenye mazingira ya namna hii, njia pekee ya kulinda utawala ni kuwabainisha wasaliti mbele ya umma kama alivyofanya Yesu ambapo aliwakusanya wanafunzi wake akawaambia kwamba “mmoja wenu atanisaliti.”
 

Baadhi ya nchi zimeweka utaratibu wa kuwatangaza wahalifu wakubwa na pengine kuwapiga risasi mbele ya hadhara.
 

Kosa kubwa kwa serikali ya Tanzania ni kuwakumbatia wasaliti, kutowaumbua 
mbele ya jamii, jambo linalowafanya wananchi waamini kuwa huwenda ufisadi ndiyo njia ambayo serikali ya awamu ya nne imeamua kupita.
 

Ameuawa mwandishi katika tukio la wazi kabisa lakini serikali ikaamua kutafuta ngonjera kupindisha ukweli: “Ooh! Alilipukiwa na bomu wakati anakimbia.”  
 

Ni mtindo wa kuteteanateteana tu. Najiuliza watakataaje wakiambiwa lao moja?
 

Kwa nini serikali inakimbia kivuli chake?  Kwa nini inajikaanga kwa mafuta yake halafu inalaumu vyama vya siasa kuwa vina mpango wa kuifanya nchi isitawalike?  Wa kulaumiwa si chama fulani cha siasa bali ni wasaliti ndani ya serikali yenyewe, huu ndiyo ukweli.
 

Serikali inalalamika nini? Mara “Oooo!  Kuna vyama vya siasa vinavyoeneza udini”.  Kwa nini visifutwe kwa sheria zilizopo? Kuna haja gani kwa waziri kulalamikia uhalifu wa watendaji bila kuchukua hatua?
 

Wananchi wakichoka kuvumilia madudu ya watendaji wa serikali wanaambiwa wanafanya vurugu. Kama serikali haitaki vurugu dawa ni moja; mali za umma zilindwe ili Watanzania wapate maisha bora kupitia rasilimali zao.
 

Mwalimu Julius Nyerere alisema katika moja ya hotuba zake kuwa, Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafua nje. Ninapotazama amshaamsha ya vyama vya siasa nahisi wananchi wameanza kutafuta mabadiliko nje ya CCM.

No comments:

Translate