Jeshi la Kenya linasema kuwa ndege zake za kivita
zimeshambulia uwanja wa ndege mjini Kismayo na kuharibu ghala yenye
silaha za wanamgambo wa Al Shabaab.
Mji wa Kismayo Kusini mwa Somalia ndio ngome kubwa ya kundi hilo ambalo lina uhusiano na Al Qaeda.
Msemaji wa al-Shabab amesema kuwa
hakuna aliyejeruhiwa wala kuuawa katika mashambulizi hayo na kwamba
hapakuwa na uharibifu wowote wa mali.
Wanajeshi wa Kenya wanashirikiana na wale wa
Muungano wa Afrika kupambana vikali na wapiganaji wa Al Shabaab ambao
wamesababisha msukosuko nchini Somalia kwa muda mrefu.
Al-Shabab wamelazimika kuondoka kutoka mji
mkuu,Mogadishu, na katika miji mingine kwa kipindi cha mwaka mmoja
uliopita ingawa bado wanadhibiti sehemu kubwa ya Kusini na maeneo ya
kati mwa Somalia.
Takriban watu 10,000 wameutoroka mji wa Kismayo katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Kwa mujibu wa shirika la kuwahudumia wakimbizi
la Umoja wa Mataifa, UNHCR idadi kubwa ya watu wameuotoroka mji wa
Kismayo huku makabiliano yakipamba moto.
Kenya ilianza harakati zake nchini Somalia mwaka
mmoja uliopita, baada ya kukithiri kwa mashambulizi kwenye mpaka wake
na Somalia ambayo Al Shabaab ililaumiwa kuyatekeleza.
Mapema wiki hii Rais wa Kenya Mwai Kibaki,
aliambia mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuwa, anatumai
wakimbizi wa Somalia wanaoishi Kenya wataweza kupelekwa katika kile
alichokiita maeneo huru ya Somalia.
Kenya inahifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi
wa kisomali katika kambi ya Dadaab waliokimbia vita na njaa nchini
Somalia katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
No comments:
Post a Comment