Wachimba migodi wa kampuni ya Lonmin nchini Afrika Kusini, wamekubali kurejea kazini siku ya Alhamisi.
Wachimba migodi hao walijawa na furaha huku
wakishangilia walipoambiwa kuhusu pendekezo la asilimia 22 la nyongeza
ya mishahara watakayolipwa.
Lakini shirika la kushughulikia
mizozo ya ajira liliambia BBC kuwa lilikuwa linasubiri ikiwa pendekezo
la hivi karibuni la mishahara litakubalika au la.
Mwezi jana polisi waliwaua kwa kuwapiga risasi
wafanyakazi wa mgodi huo waliokuwa wakigoma kudai mishahara bora na
mazingira mazuri ya kazi. Wachimba migodi 34 waliuawa.
Uzalishaji wa madini umeathirika sana kwa wiki kadhaa huku mzozo huo ukisambaa hadi katika migodi mingine.
Tume ya maridhiano iliambia BBC kwamba
waakilishi wa wafanyakazi hao, waliwashauri
wachimba migodi kuhusu
pendekezo la sasa la nyongeza ya mishahara na wala hawakupata pingamizi
zozote.
Wafanyakazi hao , walikusanyika katika uwanja mmoja karibu na mgodi wa Marikana kusikiliza hotuba ya waakilishi wao.
Wamekuwa wakidai nyongeza ya mishahara ya dola miatisa thelathini na tano. Kwa sasa wanalipwa kati ya randi 4,000 na 5,000.
''Kilichofanyika leo ni ushindi mkubwa kwa
wafanyakazi hawa na watarejea kazini siku ya Alhamisi'' alinukuliwa
akisema kasisi mmoja aliyewawakilisha wafanyakazi hao, Joe Seoka.
Pia alielezea kuwa wafanykazi hao watalipwa
randi 2,000 kwa kipindi ambacho walikuwa wanagoma kwani hawakuwa
wanapokea malipo yoyote.
No comments:
Post a Comment