Balozi wa Marekani nchini Libya amefariki baada ya
kushambuliwa na watu waliokuwa wamejihami na kuvamia ubalozi wa Marekani
Mashariki mwa mji wa Benghazi.
Balozi huyo alisemekana kuwa miongoni mwa
maafisa wengine wa ubalozi waliouawa kufuatia maandamano kuhusu filamu
iliyotolewa nchini humo ikimkejeli Mtume Muhammad.
Idara ya mambo ya ndani nchini Marekani, imethibitisha tu kifo cha afisaa mmoja wa ubalozi huo ingawa bado haijataja jina lake.
Maandamano ya kupinga filamu hiyo pia yalifanyika mjini Cairo dhidi ya ubalozi wa Marekani.
Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Hilary Clinton, amelaani mashambulizi hayo.
Serikali ya Libya imetaja shambulio hilo kama kitendo cha uoga.
Ubalozi huo uliteketezwa na watu waliojihami kwa
bunduki kulalamikia filamu moja iliyotengenezewa nchini Marekani ambayo
wanasema inamdhihaki Mtume Mohammed.
Wanamgambo hao wanaoripotiwa kuwa na ufungamano
na kundi la waislamu wenye msimamo mkali walitumia maguruneti ya
kurushwa kwa roketi kuvamia ubalozi huo kabla ya kuiteketeza. Maafisa wa
Libya wameiambia BBC kwamba hali imetulia kwa sasa.
Machafuko hayo ya Libya yalijiri saa kadhaa
baada ya maelfu ya waandamanaji kukusanyika nje ya ubalozi wa Marekani
mjini Cairo kuelezea hasira zao kuhusu filamu hiyo kumhusu Mtume
Mohammed.
Kwa wakati mmoja waandamanaji hao waliingia ndani ya ubalozi huo na kuichana bendera ya Marekani na kurejesha yao.
No comments:
Post a Comment