tangazo

Friday, September 7, 2012

Minara ya mawasiliano ya simu yashambuliwa


                                                                 Ramani ya Nigeria


 Takriban Minara 24 ya kurushia mawasiliano ya simu za mkononi imevamiwa kote nchini Nigeria.

Msemaji wa jeshi ameripotiwa akilaumu kundi la wapiganaji la Boko Haram kwa uvamizi huo wa kwanza wa aina yake dhidi ya kampuni tisa za huduma za simu.
Kundi la Boko Haram limekuwa likilaumu kampuni hizo kwa kushirikiana na mashirika ya usalama kuwasaka wanachama wa kundi hilo.

Wataalamu wanasema kuwa uharibifu huo utagharimu kampuni hizo mamilioni ya dola.

Milio ya risasi na milipuko ilisikika huku moto mkubwa ukiteketeza minara hiyo Mjini Kano sawa na miji ya Maiduguri, Gombe na Bauchi.

Uvamizi mwingine ulitokea mjini Potiskum.
Msemaji wa jeshi mjini Maiduguri Luteni Kanali Sagir Musa, aliambia BBC kuwa maafisa wa usalama walishuku kundi la Boko Haram kwa uvamizi huo.

Kwa mujibu wa Luteni Kanali Musa, hii ni mbinu mpya ya mashambulizi ambayo imeanza kutumiwa na kundi hilo.

Siku ya Jumatano, kampuni tisa ziliripoti uharibifu uliofanyiwa minara yao 24. Duru zinaarifu kuwa baadhi ya kampuni zilizolengwa ni MTN ya Afrika Kusini pamoja na ile ya himaya ya nchi za kiarabu, Etisalat.

Boko Haram lilianza kufanya mashambulizi mwaka 2009 wakitaka sheria za kiisilamu kutumika, wakishambulia majengo ya serikali , makanisa na kuwaua wahubiri wa kiisilamu wenye msimamo wa kadri.

No comments:

Translate