Julius Malema amewaambia wafuasi wake kuwa katu hatishiki na uamuzi wa mahakama kusema kuwa ana kesi ya kujibu.
Mahakama hii leo ilimwachilia kwa dhamana Malema anayekabiliwa na shtaka la kuhaulisha pesa.
Malema ambaye aliwahutubia wafuasi
wake nje ya mahakama, pia anatuhumiwa kwa kutumia nafasi yake ya zamani
kama kiongozi wa tawi la vijana la ANC kujitajirisha yeye na washirika
wake wa biashara.
Washirika wake wengine wanne nao walikabiliwa na mashtaka sawa na hiyo katika kesi yao iliyosikilizwa hapo jana.
Katika hotuba yake kwa mamia ya wafuasi wake nje
ya mahakama mjini Polokwane, bwana Malema alisema ataendelea na juhudi
zake za kutetea maelefu wanaoishi katika umaskini nchini humo.
Seng'enge zilizungushwa katika eneo la mahakama hiyo iliyopo Polokwane, mji mkubwa wa jimbo analotokea mwanasiasa huyo,Limpopo.
Wafuasi wake wanasema mashtaka hayo yameshinikizwa kisiasa.
Wakiimba na kucheza nje ya mahakama hiyo wafuasi
wengi wa chama hicho cha ANC tawi la vijana walishikilia mabango
yaliosema 'Muacheni kiongozi wetu'.
Maafisa wa usalaman walidhibiti ulinzi na kulikuwa na utulivu mkubwa.
Julius Malema na washirika wake wa kibiashara
wanashutumiwa kwa kufaidi kutokanana na mikataba ya serikali katika
jimbo la Limpopo, tuhuma ambazo anazikana. Mwanasiasa huyo mwenye umri
wa miaka 31 pia anachunguzwa
katika kesi tofauti ya ukwepaji kulipa
ushuru.
Malema ni maarufu sana Afrika Kusini kwa
ukakamavu wake wa kutetea maslahi ya wananchi na maisha yake ya
kifahari, huku akijitambulisha kama mpiganiaji uhuru wa uchumi.
Alitimuliwa kwenye chama hicho tawala mnamo mwezi Aprili akishutumiwa kwa kuzusha migawanyiko katika chama hicho.
Ni mkosoaji mkali wa a Jacob Zuma, hivi karibuni
akimshutumu rais huyo kwa alivyoushughulikia mgomo wa wachimba migodi
wa Marikana.
Kwa mujibu wa mwandishi wa masuala ya Afrika,
Andrew Harding, baadhi ya watu Afrika kusini wanaamini anafikishwa
haraka mahakamani, ikiwa ni chini ya wiki moja baada ya kutolewa waranti
ya kukamatwa kwake, ili kuimarisha nafasi ya kisiasa ya Zuma.
Mwandishi wetu anaeleza kwamba huenda ikawa ni
kesi ya muda mrefu, ambayo huenda ikatoa nafasi ya kujulikana ukweli
kuhusu suala hilo la rushwa, ambalo watu wengi wanaamini inaitia nchi
hiyo doa.
No comments:
Post a Comment