tangazo

Tuesday, July 24, 2012

Balozi Seif Idd Azungumza Na Wanahabari Kuhusu Kuzama Kwa Mv. Skagit


Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuunda Tume ya uchunguzi wa ajali ya Mv. Skagit iliyozama July 18 mwaka huu ambapo jumla ya abiria 290 walikuwemo katika meli hiyo.

Balozi Seif ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni kuhusiana na kuzama kwa meli hiyo.

Amesema Tume hiyo itaweza kuishauri Serikali nini cha kufanya katika kuhakikisha kuwa vyombo ambavyo vinachukuwa abiria vinakuwa vya aina gani na kuweka utaratibu mzuri utakaoweza kufanikisha usafiri wa baharini.

Ameongeza kuwa kutokana na hali ya ajali zinazotokea mbali na Tume hiyo,Serikali imeona kuwa ipo haja ya  kupitia sheria zinazohusu usafiri wa baharini na kuweka aina ya viwango vya meli zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini na kuchukua abiria.

Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa nia ya Serikali juu ya ununuzi wa Meli kwa ajili ya usafiri ipo pale pale na kwamba juhudi zinaendelea katika kufanikisha suala hilo.

Akizungumzia kuhusu ajali hiyo Balozi amefahamisha kuwa jumla ya watu 146 mpaka sasa wameokolewa wakiwa hai ambapo Maiti 78 zilipatikana wakiwemo wanaume,wanawake na watoto.

Aidha amesema kuwa Chombo hicho kilikuwa na Raia wa kigeni 17 na waliookolewa wakiwa hai ni 15 mmoja amepatikana akiwa amefariki ambaye ni Raia wa Uholanzi na mmoja mpaka sasa hajapatikana.

Wageni hao kutoka nchi za nje ni wa Ubelgiji,Marekani,Ujerumani,Uholanzi pamoja na Israel na Serikali imetoa huduma kwa wageni hao na tayari wameondoka kurudi makwao kwa salama.

Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi alieleza kuwa kati ya majeruhi 138 waliopelekwa Hospitali kuu ya Mnazimmoja iliyopo mjini Zanzibar kwa uchunguzi hadi kufikia leo wagonjwa wote hao walikwisharuhusiwa baada ya kupata matibabu.
Amewataka wananchi popote pale ambapo wataiona maiti wapeleke taarifa kwa Jeshi la Polisi,Wakuu wa Wilaya,Mikoa na Masheha ili taratibu za kuihifadhi maiti hiyo ziweze kuchukuliwa.

Amesema kuwa zoezi la uokoji linaendelea na kuwashukuru wananchi Vikosi vya ulinzi vya Tanzania na vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na vyombo binafsi na wazamiaji kutoka nchi za nje kwa ushirikiano walioutoa uliofanikisha kwa kiasi fulani shughuli hiyo ya uopoaji wa maiti hizo.

No comments:

Translate