tangazo

Tuesday, July 10, 2012

LUBANGA AHUKUMIWA MIAKA 14 GEREZANI

Mbabe wa kivita kutoka Congo, Thomas Lubanga, amehukumiwa kifungo cha miaka 14, baada ya kupatikana na hatia ya kuwasajili watoto katika jeshi lake kati ya mwaka wa 2002 na 2003.


Lubanga alipatikana na hatia na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC mwezi Machi mwaka huu.
Hukumu hiyo ndiyo ya kwanza kutolewa na mahakama hiyo ya ICC iliyoundwa miaka 10 iliyopita.

Lubanga amekanusha mashtaka yote dhidi yake akisema hakuna kosa alilofanya na kwamba hakuunga mkono watoto kutumiwa kama wanajeshi.

Lakini majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo, walikubaliana kwa kauli moja kuwa Lubanga alikuwa na hatia.

Zaidi ya watu 60,00 waliuawa

Shirika la kutetea haki za kibinadam, la Human Rights Watch, limedai kuwa zaidi ya watu 60,000 waliuawa kwenye mzozo kati ya watu ya kabila la Hema na Lendu, mkoani Ituri, Kaskazini Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mwezi juni mwaka huu, aliyekuwa mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo ICC, Louis Moreno Ocampo aliomba mahakama hiyo kumhukumu bwana Lubanga zaidi ya miaka 30 gerezani.

Kuhukumiwa kwa bwana Lubanga kumehusishwa na machafuko yanayoendelea nchini Congo.
Wanajeshi wa waasi wanaopinga serikali wamekaribia mji wa Goma Mashariki mwa nchi hiyo.

Kiongozi wa waasi hao ni Generali Bosco Ntaganda, ambaye pia anasakwa na mahakama hiyo ya ICC.

No comments:

Translate