Katibu mkuu wa chama cha demokrasia na maendeleo.(chadema)
Waziri nchimbi
ATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt.
Willibroad Slaa, amesema pamoja na madai waliyotoa kwa Serikali juu ya
kuandaa mkakati wenye lengo la kuwateka, kuwadhuru baadhi ya viongozi
wake kitaifa, hawapo tayari kuhojiwa na Jeshi la Polisi kama alivyoagiza
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Alisema msimamo huo unatokana na chama hicho
kutokuwa na imani na jeshi hilo ambalo kwa nyakati tofauti, limeshindwa
kushughulikia malalamiko ya chama hicho ambayo wamekuwa yakiyapeleka kwa
masilahi ya Taifa.
Dkt. Slaa aliyasema hayo Dar es Salaam jana
wakati akizungumza na waandishi wa habari siku moja baada ya Dkt.
Nchimbi, kuliagiza Jeshi la Polisi kuwahoji baadhi ya viongozi wake
waliodai Serikali imeanda mkakati huo ambao unaratibiwa na Usalama wa
Taifa.
Mbali ya Dkt. Slaa, viongozi wengine waliodai kuandaliwa
mkakati huo ambao Dkt. Nchimbi, aliagiza wahojiwe na polisi ni pamoja na
aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbress Lema na Mbunge wa
Ubungo, Bw. John Mnyika.
“Tumechoshwa na tabia ya Jeshi la Polisi
kupuuza malalamiko mbalimbali ambayo tunawapelekea juu ya kutoridhishwa
na baadhi ya mambo yanayogusa masilahi ya Taifa hivyo hatupo tayari
kuhojiwa wala hatuoni sababu ya kujipeleka vinginevyo tupo tayari
kukamatwa,” alisisitiza Dkt. Slaa.
Alisema Kamati Kuu wa CHADEMA
ambayo ilikutana jana, ililaani hatua ya viongozi wake kupokea vitisho
ambavyo vinahatarisha usalama wa maisha yao.
Aliongeza kuwa,
pamoja na vitisho hivyo, tayari amepokea simu kutoka kwa mtu mmoja
aliyejitambulisha kuwa Ofisa wa Polisi kutaka akutane naye.
“Nilichomwambia
ni kwamba, sina muda huo na sipo tayari kukutana naye wala mtu mwingine
yeyote,” alisema Dkt. Slaa akipinga agizo la Dkt. Nchimbi, kutaka
polisi iwahoji.
“Dkt. Nchimbi hakustahili kutoa agizo kama hili
badala yake wao walipaswa kuichunguza Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi
la Polisi ndiyo maana Wizara hii inapewa bajeti kubwa kwa ajili ya
mambo kama haya.
“Wizara hii inatengewa fedha nyingi kwa ajili ya
mambo kama haya hivyo lazima yachunguzwe kwa kina badala ya kutoa kauli
zisizo na tija, umaaarufu wa chama chetu na sisi wenyewe hautokani na
siasa bali ni kukubalika na wananchi si vinginevyo,” alisema Dkt. Slaa.
Katika
hatua nyingine, chama hicho kimetangaza ratiba yake ya kujikita katika
mikoa mitano siku 44 kwa ajili ya kujiimarisha na kuhamasisha wananchi
kukiunga mkono.
Alisema mikutano hiyo imepewa jina la “Operesheni
Sangara” chini ya kauli mbiu inayosema; “Hakuna kulala, hakuna kula,
hakuna kunywa hadi kieleweke”.
Dkt. Slaa alisema miongoni mwa
mikoa inayolengwa kwenye operesheni hiyo pamoja na Singida, Dodoma,
Tabora, Shinyanga na watafika vijiji 4,000, kata 806 na majimbo 44,
kwani lengo cha chama hicho ni kuongoza Serikali.
No comments:
Post a Comment