Afisaa mkuu kabisa kujiondoa
katika serikali ya rais wa Syria, Bashar al Assad, ameambia BBC kuwa
utawala wa Assad hautahofia kutumia zana za kemikali ikiona tisho kubwa
dhidi yake kutoka kwa upinzani.
Nawaf Fares, balozi wa zamani wa Syria nchini
Iraq, alisema kuwa taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa huenda
zana hizo tayari zimetumiwa.Aliongeza kuwa mashambulizi ya mabomu ambayo yameshuhudiwa nchini humo, yamefanywa na utawala wa Assad kwa ushirikiano na wapiganaji wa Al-Qaeda.
Wakati huohuo,mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa na jumuiya ya nchi za kiarabu kuhusu mzozo wa Syria Kofi Annan, anatarajiwa kukutana na rais wa Urusi, Vladimir Putin kuhusiana na mzozo huo wa Syria.
Urusi ni mshirika mkubwa wa Syria na mkutano huu unakuja wakati shinikizo zikiendelea kukuthiri kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali dhidi ya Syria.
Syria imeshuhudia mzozo wa kisiasa tangu mwezi Machi mwaka jana wakati harakati za mapinduzi ya kiraia zilipoanza dhidi ya utawala wa Bashar al-Assad.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa,Ban Ki-Moon anatarajiwa nchini Beijing kwa mazungumzo na rais wa nchi hiyo ambayo imejiunga na Urusi kupinga vikwazo vyovyote dhidi ya utawala wa Assad kwa kutumia kura yao ya turufu.
Juhudi za kidiplomasia zinajiri wakati maafisa wa umoja wa mataifa nchini Syria wakilalamika kuhusu vizingiti vikubwa katika juhudi zao za kutoa msaada kwa watu waliokwama katika maeneo ya vita.
Syria inajulikana kwa kuwa na zana nyingi za kemikali. Wasiwasi umekithiri katika nchi jirani za Syria na katika baadhi ya nchi za magharibi kuhusu usalama wa zana hizo ikiwa utawala wa Asaad utaporomoka.
Alipoulizwa uwezo wa rais Assad kutumia zana hizo dhidi ya upinzani, bwana Fares aliambia BBC katika mahojiano naye kuwa hilo linaweza kufanyika akimtaja rais Assad kama mtu aliyejeruhiwa na pia
kumfananisha kama mtu aliyenaswa.
Fares aliambia BBC kuwa rais Assad anaweza tu kuondolewa mamlakani kwa nguvu.
"kuna taarifa ambazo bado hazijathibitishwa kuwa zana za kemikali tayari zimetumiwa dhidi ya wapinzani hasa katika mji wa Homs," alisema Fares.
Madai yake kuwa wapiganaji kutoka madhehebu ya Sunni wanashirikiana na Al-Qaeda pamoja na wapiganaji wengine wa madhehebu ya Allawite ambao ndio wengi zaidi katika utawala wa Assad kupigana dhidi ya upinzani huenda yakawashangaza wengi.
Ghasia zingali zinaendelea kuenea katika maeneo mengi ya nchi na hata katika mji mkuu Damascus huku waasi ambao sasa wamejihami vya kutosha pamoja na kuwa wana mwelekeo mzuri , wakipambana na wanajeshi pamoja na makundi ya wapiganaji wa serikali.
Inaarifiwa kuwa mji mkuu sasa unashuhudia idadi kubwa zaidi ya wanajeshi wanaoshika doria tangu kuanza kwa harakati hizi miezi kumi na sita sasa imepita.
Wanaharakati wameripoti kutokea makabiliano kusini magharibi mwa mji mkuu na kusema kuwa mapigano mapya yamezuka katika maeneo ya Barzeh na Qaboun. Watu kumi waliuawa mjini Damascus ikiwa ni idadi ndogo kuliko iliyoshuhudiwa katika miji ya Hama na Homs.
No comments:
Post a Comment