Chifu merere 11 Wa kabila la masangu
CHIFU
Merere II (70) (pichani) wa kabila la Wasangu, ameokolewa na polisi
kuzikwa akiwa hai baada ya kutokea tafrani katika msiba wa kijana
aliyefahamika kwa jina moja la Frank mkazi wa Kijiji cha Ijumbi, Kata ya
Ruiwa, wilayani Mbarali mkoani hapa.
Tukio hilo lilitokea baada ya
chifu huyo kutuhumiwa kushirikiana na ndugu wa marehemu kwenda kupiga
ramli ya ugonjwa wa kijana huyo kabla ya kifo kwa mganga wa kienyeji
ambaye jina lake halikutajwa wa Mbozi mkoani hapa, aliyeagiza kuchinjwa
ng’ombe mmoja na kupikwa pombe ya kienyeji debe 12 kwa maelezo kuwa
mgonjwa angepona.
Kufuatia agizo hilo la mganga, marehemu aliuza
shamba kwa shilingi 450,000 kisha fedha hizo kumkabidhi Chifu Merere II
kwa ajili ya tambiko na baadaye ng’ombe alichinjwa, pombe ikapikwa na
kuitwa baadhi ya wanandugu mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka.
Mganga alidai kuwa waliomroga mgonjwa wao ni ndugu wa karibu na majirani licha ya kutoweka wazi majina yao.
Sakata
la Chifu Merere II kutaka kuzikwa akiwa hai limekuja baada ya Frank
kufariki dunia Julai 10, mwaka huu na vijana wa Kijiji cha Ijumbi kutaka
maelezo kwa nini marehemu alifariki wakati tayari tambiko lilifanyika
na fedha zake kuliwa.
Haikuishia hapo, vijana hao waligoma kuchimba
kaburi na kumtaka chifu huyo arudishe fedha vinginevyo atazikwa yeye
akiwa hai ili iwe fundisho.
Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Jordan
Masweve alipopata taarifa hizo alienda nyumbani kwa chifu na kukuta
vijana wamemzonga wakimdai fedha zilizotumika katika tambiko ndipo
kiongozi huyo alipomchukua na kwenda kumfungia katika mahabusu ya
kijiji.
Wanakijiji walichimba kaburi la Frank baada ya kuombwa hivyo
na mtendaji huyo, baada ya kumzika marehemu vijana waling’ang’ania
kutaka Chifu Merere azikwe hai ndipo taarifa zilipofika polisi na
haraka, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Diwani Athuman alipotuma
askari kijijini hapo kwa ajili ya kumwokoa kiongozi huyo wa kimila.
Baada
ya mazungumzo marefu, Chifu huyo aliweza kurejesha shilingi 350,000 za
shamba lililouzwa na akaahidi kiasi kilichobaki kitapatikana siku chache
zijazo ndipo aliachiwa huru saa 12 jioni.
Mwanamke mmoja wa Kijiji
cha Malamba kata hiyohiyo, Rozina Mwadala(60), alizikwa akiwa hai Juni
2, mwaka huu baada ya mganga huyohuyo wa kienyeji kutoka Mbozi kudai
ndiye aliyesababisha kifo cha Frank Lingo (25), aliyefariki Juni Mosi
mwaka huu kwa kuugua sikio.
No comments:
Post a Comment