tangazo

Friday, July 6, 2012

KOCHA MPYA WA YANGA AMUULIZIA REFA.

                                                      Kocha mkuu mpya wa Yanga, Tom Saintfiet.   

  SIKU moja baada ya kutua Jangwani, kocha mkuu mpya wa Yanga, Tom Saintfiet ameanza kazi kwa kuonyesha kuwa anawajua vizuri kiungo, Haruna Niyonzima na beki, Stephano Mwasyika huku akijinadi kuwa anahitaji makombe yote ambayo timu yake itashiriki.
Saintfiet raia wa Ubelgiji alitua mazoezini kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini Dar es Salaam ambapo wakati wa utambulisho alionyesha kuwajua zaidi wachezaji hao kwa kutoa taarifa ambazo zinawahusu.
Mara baada ya Niyonzima kujitambulisha mbele ya kocha huyo alimwambia: “Wewe ndiye ambaye unajua kuzungumza Kifaransa eeh!” Niyonzima akajibu: “Ndiyo.” Wakati kwa Mwasyika alimuuliza: “Nina taarifa zako, wewe si ndiyo ulimpiga refa?”
Swali hilo llisababisha vicheko kutoka kwa wachezaji wengine na ndipo beki huyo aliyekuwa amesimama, alikaa chini bila kujibu chochote huku akitabasamu, likionekana ni swali lililozua mshituko kutokana na kocha huyo mgeni kujua tukio la Mwasyika kumpiga mwamuzi, Israel Nkongo, msimu uliopita.
Utambulisho huo ulipomalizika, Kocha Msaidizi wa Yanga, Felix Minziro alipanga timu iliyocheza dhidi ya Shein Rangers ya Sinza na kupata ushindi wa mabao 5-1. Saintfiet alisema:

“Nimefurahishwa na viwango vya wachezaji na nitashirikiana vema na Minziro, kuandaa timu.”
Kuhusu Simba, alisema: “Naifahamu Simba muda mrefu, siwafikirii kabisa kwa sasa na sitaki kuwazungumzia kwa kuwa naelekeza nguvu kwenye kikosi changu.”
Aidha, alisema anawahitaji mazoezini wachezaji wa timu hiyo walio katika kikosi cha taifa chini ya miaka 20, Serengeti Boys, ambao ni Omega Seme, Frank Domayo na Simon Msuva ili kuona viwango vyao.
Katika hatua nyingine ‘injini’ ya usajili ya Yanga, Seif Magari ameliambia Championi Ijumaa kuwa jana saa saba mchana kocha huyo alitarajia kusaini mkataba wa miaka miwili ya kuifundisha timu hiyo.

No comments:

Translate