Askari wa Jeshi la wananchi(JWTZ)wakiwa katika Bandari ya Zanzibar
wakisubiri bila mafanikio miili ya watu walizozama na Meli ya Mv. Skagit
kabla ya zoezi hilo kusitishwa rasmi na Serikari kupitia kwa makamu wa
Pili wa Raisi Seif Ali Iddi jana
SERIKALI imesitisha rasmi zoezi la uokoaji wa miili ya watu waliozama
katika ajali boti ya Mv Skagit Jumatano iliyopita kutokana na ugumu wa
kazi hiyo, huku miili zaidi ya 76 ikipotea baharini. Makamu wa Pili wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd
alisema hayo wakati akipokea msaada kutoka Benki ya NMB kwa ajili ya
waathirika wa ajali hiyo.
Alisema wataalamu waliokwenda kwenye eneo la ajali kwa ajili ya
uokoaji wamethibitisha kutopata mwili hata mmoja kwa muda siku mbili,
hivyo Serikali imeamua kusitisha zoezi hilo.
“ Tumeamua siku ya kesho (leo) kusoma hitima kwenye misikiti yote ya
Unguja na Pemba, lakini kitaifa hitima hiyo itasomwa katika Msikiti wa
Mwembeshauri eneo la Rahaleo mjini Zanzibar,” alisema.
Alisema hitima hiyo itafanyika kwenye misikiti mikuu na kwamba katika
mikoa yote hitima hiyo itafanyika saa 7.00 baada ya Sala ya Adhuhuri.
Kabla ya kauli hiyo ya Serikali, Jana ilikuwa siku ya nne kufanyika
kwa zoezi la kutafuta maiti katika Bahari ya Hindi lakini waokoaji
walirejea majira ya jioni bila ya maiti yoyote.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema
waliokwenda katika uokozi huo walirejea bila kupata maiti hata moja.
Kati ya watu 290 waliokuwa wamepanda kwenye boti hiyo, ni 146 ndio
waliookolewa wakiwa hai huku maiti 68 zikiopolewa baharini ambapo Kaimu
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Vyombo vya Baharini,
Abdalah Hussein
Kombo alisema pia zoezi la uokoaji ni gumu.
Awali, mmoja wa wazimiaji ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe,
alisema : “ Meli inaonekana lakini namna ya kuipindua ili kuziondoa
maiti zilizopo tumeshindwa kwa sababu ya ukosefu wa vifaa.”
Katika hatua nyengine Chama cha NCCR-Mageuzi, kimetaka mfumo wa
vyombo vya usafiri katika visiwa vya Zanzibar na Pemba kuangaliwa upya
ili kuepusha maafa zaidi kutokana na ukweli kuwa hata ndege zinazofanya
safari zake katika visiwa hivyo na Dar es Salaam zina walakini.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema, licha ya boti na
meli ambazo hazipo katika viwango vya usalama lakini pia ndege
zinazofanya safari kati ya Pemba na Dar es Salaam usalama wake ni wa
mashaka.
Akizungumzia usafiri wa ndege alisema, mafuta hunuka katika sehemu ya
abiria na kuongeza kuwa ni wazi kuwa ndege ya namna hiyo inaweza
kulipuka wakati wowote na alienda mbali zaidi kwa kueleza kuwa ndege
hizo ndogo nyingi milango yake mibovu.
“Niliwahi kupanda ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Pemba, mlango
unagonga gonga na nilipouliza niliambiwa na rubani kuwa kesho
utatengenezwa ni kitasa ndio kimeharibika”, alisema Ruhuza na kuongea
kuwa hana uhakika kama ndege hizo huwa zinakaguliwa na hilo ni jambo la
hatari kuendelea kubaki kama ilivyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii, Constantine Akitanda alisema,
kilichotokea Zanzibar ni matokeo ya rushwa kwani chombo hicho kilipigwa
marufuku kubeba abiria nchini Marekani lakini fedha zilitumika,
ikachakachuliwa Mombasa kisha ikaletwa Zanzibar kufanyakazi jambo ambalo
limegharibu roho za watu.
Alisema hali hiyo pia ni matokeo ya watendaji wa Serikali kutaka
kufanyabiashara na kufanya siasa vitu ambavyo daima haviwezi
kuchanganyika na ikitokea basi matokeo yake huwa kama ilivyotokea
Zanzibar.
“Rushwa ndiyo matokeo ya ajali ile, kwani wasimamizi wa sheria na
sera ndiyo wafanyabiashara hivyo wanashindwa kunyoosheana vidole na
matokeo yake roho za watu zinapotea na ajali ambayo ni ya tatu kwa meli
ambazo zinamilikiwa na kampuni hiyo.
Alisema ajali ya kwanza ilikuwa ya meli yao moja iitwayo Mv Fatah
ambayo ilizama bandarini kabla haijaondoka na zingine ndio hizo mbili
ambazo zimechukua roho za mamia ya watu na kuonya kuwa hatua za maana
zisipochukuliwa Taifa kila mara litakuwa katika kazi ya kutafuta miili
ya watu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democtaric Change (ADC), Dawi
Kadawi Limbu alisema sera ya Serikali ya kujiondoa katika biashara
zikiwamo za huduma muhimu ndiyo chanzo cha matatizo haya kwani sasa roho
za watu zinashikwa mikononi mwa wafanyabiashara ambao wanaweza kuamua
chochote wanachotaka wao.
“Kuna huduma Serikali haiwezi kukwepa kuzitoa ikiwa ni pamoja na za
usafiri wa reli, majini na usafiri wa mabasi” alisema na kuongeza kuwa
kuziacha huduma hizo muhimu mikononi mwa wafanyabiashara kwa kisizingizo
kuwa serikali haifanyabiashara ni uvivu wa kufikiri.
Alisema dunia nzima suala la huduma za usafiri licha ya kuwapo watu
binafsi pia Serikali inatoa ili kuwahakikishai usalama wananchi wake na
ameshangaa kuiona Serikali ikishindwa kujifunza kutokana na ajali za
majini.
“Mv Bukoba ilipoua mwaka 1999 tulidhani Serikali imejifunza kitu
lakini cha ajabu hakuna kitu kama hicho na Ziwa Victoria ajali nyingine
itarajiwa wakati wowote kwani meli ya Mv Victoria bado inafanyakazi kati
ya Bukoba na Mwanza licha ya uchakavu wake”, alisema.
No comments:
Post a Comment