tangazo

Saturday, July 21, 2012

BI. HARUSI AFA BWANA HARUSI APONA





HUKU majonzi yakiwa bado yametawala miongoni mwa Watanzania kufuatia vifo vya watu waliokuwa ndani ya meli ya MV Skagit ambayo ilipinduka na kuzama Julai 18, 2012 karibu na Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar mambo mengi yameibuka.
Nje ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik siku ya Jumatano (juzi) ambako serikali ilikuwa ikitoa ripoti ya maendeleo ya uokoaji, baadhi ya watu walikuwa katika hali ya majonzi kufuatia ndugu zao kutojulikanna walipo.
Hamis, aliyedai ni mfanyakazi wa Kampuni ya Azam ya tajiri Said Salim Bakheressa alisema mdogo wake, Khalfan na mchumba wake, Zaina Ally walikuwa ndani ya meli hiyo kwenda Zanzibar kufunga ndoa Alhamisi (juzi) kama maandalizi ya kuukaribisha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, lakini mpaka siku hiyo mdogo wake aliokolewa, ila Zaina hajulikani alipo.
Hamis alisema: “Naamini shemeji yangu amefariki dunia, kwani katika watu wote waliokolewa hayupo, maskini mdogo wangu (Khalfan), alikuwa akafunge ndoa ili wakati wa swaumu mkewe awe halali kumpikia chakula.”
Akaongeza: “mbaya zaidi, mpaka muda huu (saa saba mchana Alhamisi) serikali imetangaza kupatikana kwa miili mingine nane, lakini pia shemeji yangu hayupo.”
Hamis aliongeza kuwa ndoa hiyo ilikuwa ifungwe jijini Dar wiki iliyopita, lakini wazazi wa Zaina ambao wote wanafanya kazi serikalini Zanzibar waliomba ikafungwe visiwani humo.
MENGINE YA KUSHANGAZA
Mtu mwingine ambaye hakutaja jina lake, alisema siku ya tukio, yeye alimsindikiza mdogo wake mpaka bandarini, akiwa anapanda meli hiyo, yeye akaondoka kuendelea na shughuli zake.
“Sasa niliposikia meli imezama, nikampigia simu, hakupatikana, nikajua tayari. Nilituma habari kwa ndugu mbalimbali tayari kwa maandalizi ya msiba.
“Lakini ilipofika saa kumi na mbili jioni akanipigia simu akiniuliza kama nimesikia kuna meli imezama. Nilishtuka, nikahisi naongea na mzimu, nilipomuuliza ameponaje akasema alighairi akapanda meli nyingine, alipofika Zanzibar simu yake ikazima kwa sababu ya kuishiwa chaji.”
Naye mzee Fasha Abduel, mkazi wa Magomeni, jijini Dar, alisema siku hiyo ya tukio, asubuhi alimpeleka bandarini mtoto wa mdogo wake aitwaye Shaban na alimkatia tiketi kwenye meli hiyo, lakini kijana huyo alikuwa hataki kwenda Zanzibar ambako ndiko aliko baba yake mzazi.
“Kumbe nilipoondoka kwenda kazini kwangu (Manispaa ya Temeke) na yeye akageuza kurudi nyumbani. Ajali ilipotokea nilishtuka sana, nikampigia simu mdogo wangu kule Zanzibar, akaanza kilio. Nilipompigia mke wangu kumjulisha, akasema mbona Shaban alirudi muda uleule wa asubuhi na amejaa tele nyumbani,” alisema mzee huyo.
Mzee Hassan, mkazi wa Kariakoo, jijini Dar, yeye alikuwa akipeleka magunia matupu Zanzibar, lakini asubuhi wakati akijiandaa, mwanaye wa kiume, Ally anayesoma Shule ya Msingi Makurumla, Dar aliugua ghafla, hivyo ikabidi yeye akatume magunia hayo kwenye meli hiyo na kumtaarifu mtu wa kuyapokea Bandari ya Malindi, Zanzibar ikawa salama yake.
HALI HALISI
Mpaka tunakwenda mitamboni, maiti zilizopatikana kufuatia ajali hiyo ni 31 huku 146 wakiwa wameokolewa na 117 hawajulikani walipo.
MELI YAFIKA MITA 47
Habari zaidi zisema kuwa, meli hiyo ambayo ilizama jumla jioni ya Jumatano, ilifika kina cha mita 47 kwenda chini wakati uwezo wa wazamiaji waliokuwa kwenye eneo la tukio ni mita 30 tu.
SPIKA WA BUNGE AWARUHUSU WABUNGE KWENDA MISIBANI
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda, Julai 19, aliahirisha bunge na kuwataka waheshimiwa waende misibani kuungana na Watanzania wengine katika kipindi hiki kigumu.
SIKU 3 ZA MAOMBOLEZO ZAISHA LEO
Wakati serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikitangaza siku tatu za maombolezo ambapo bendera hupepea nusu mlingoti, juzi Alhamisi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano nayo ikatangaza siku tatu za maombelezo kwa nchi nzima ambazo zinakwisha leo.
KWA NINI KUTOKA DAR?
Kumbukumbu za haraka zinaonesha kuwa, sehemu kubwa ya ajali za meli hutokea wakati wa kutoka Dar kwenda Unguja au Pemba.
Miezi kumi iliyopita, Meli ya MV Spice Islanders ilipata ajali ikiwa inatoka Dar, kupitia Unguja kwenda Pemba.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema hata meli nyingi zinazozima injini majini, nyingi huwa zinatoka Dar kwenda Unguja.
UITABIRI WA MAAFA KUONGEZEKA
Wakati hayo yakitokea, baadhi ya Watanzania wametabiri ajali zaidi za meli wakidai kuwa nyingi haziko vizuri kwa safari za majini.
“Kama serikali haitachukua hatua ya kukagua meli zetu, ajali nyingi mbele zinakuja kwani meli nyingi hazina sifa ya kufanya safari za majini kutokana na kuzeeka au kutofanyiwa matengenezo.
KUTOKA KWA MHARIRI
Mungu awatie nguvu na uvumilivu wale wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo. Tuliwapenda wapendwa wetu, lakini Mungu amewapenda zaidi. Amina.

No comments:

Translate