MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewaachia huru wafungwa watatu
waliokuwa wakitumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kuhujumu
miundombinu ya mawasiliano ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Wafungwa
hao walioachiwa ni Naclis Thomas, Charles na Mshamu Mbowela.
Walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu Agosti 29, mwaka jana baada ya kuwatika hatiani kwa makosa matatu
ya kula njama, kuvuruga na kutumia isivyo halali mifumo ya mawasiliano
ya TTCL.
Lakini, jana Mahakama Kuu iliwaachia huru baada ya
kubaini kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikosea katika kutoa
adhabu, baada ya washtakiwa hao kukata rufaa wakipinga hukumu na adhabu
hiyo. Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Dk Fauz Twaib, kwanza alitupilia
mbali hoja za rufaa ya warufani hao akisema hazina msingi na kwamba,
mwenendo wa kesi ya msingi ulikuwa sawa.
Pia, Jaji Dk Twaib
alisema anakubaliana na hoja za Wakili wa Serikali Mhina wakati wa
usikilizaji wa rufaa hiyo kuwa, ushahidi uliowatia hatiani ulikuwa
unajitosheleza na haukuhitaji ushahidi zaidi wa kuunga mkono, kama
warufani walivyodai.
Hata hivyo, akihitimisha hukumu yake
alikubaliana na hoja ya Wakili wa Serikali kuwa, Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu ilikosea katika kutoa adhabu kwa kuwa adhabu waliyopewa
warufani hao haikuwa sahihi. “Sikuona tatizo lililoharibu mwenendo wa
kesi ya msingi kama warufani walivyodai.
Jambo ambalo lingeweza
kuwasaidia ni kwamba Hakimu Fimbo (Sundi, aliyewahukumu adhabu hiyo)
hakutaja kifungu cha sheria alichokitumia kutoa adhabu hiyo,” Jaji Dk
Twaibu alisema na kuongeza:
“Hata hivyo, tatizo hilo
linarekebishika chini ya kifungu cha 388 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai (CPA).” Jaji Dk Twaib alisema kosa la kwanza na la pili
ndiyo makosa makubwa, ambayo adhabu yake ni faini ya Sh300,000 au
kifungo cha miaka mitatu jela au vyote viwili kwa pamoja.
Kuhusu
kosa la kwanza la kula njama, Jaji Dk Twaib alisema adhabu yake ni
kifungo cha miaka saba jela, lakini akasema katia kutoa adhabu inabidi
makosa makubwa pia yaangaliwe.
“Kisheria mahakama haina budi
kuanza na adhabu ya faini, lakini hakimu alitoa adhabu ya kifungo moja
kwa moja, hii si sahihi alipaswa aangalie kifungu cha faini kwanza,”
alisema Jaji Dk Twalib na kuongeza:
“Hata kama aliona kifungu cha
adhabu ya kifungo jela basi alipaswa aangalie kifungu kinachopunguza
adhabu.” Alisema anakubaliana ilikuwa sahihi kuwatia hatiani kwa makosa
hayo, lakini akaondoa adhabu ya kifungo itakayopelekea warufani
kuachiliwa huru mara moja.
No comments:
Post a Comment