tangazo

Monday, July 16, 2012

TIMU ZA SIMBA NA YANGA ZAANZA VIBAYA KOMBE LA KAGAME.










 DANNY Mrwanda alikuwa katika wakati mgumu jana, wakati Simba ilipochezea kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya URA ya Uganda katika mchezo wa Kombe la Kagame uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 

Mshambuliaji huyo aliyetua Msimbazi hivi karibuni akitokea katika klabu ya DT Long An ya Vietnam, alijikuta akizomewa na mashabiki wa Simba kwa kile walichodai kuwa hakuwa akikaba na alipoteza pasi nyingi, hali iliyomlazimu kocha Milovan Cirkovic amtoe na nafasi yake kuchukuliwa na Abdallah Juma.

Simba walitarajia kuondoka uwanjani hapo vifua mbele, hasa kwa kuwa jana yake watani wao wa jadi, Yanga walichezea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Atletico ya Burundi, lakini hali haikuwa kama ilivyotarajiwa.

Mabao mawili ya mshambuliaji Sheni Ali, dakika ya 12 na 90, yalitosha kabisa kuwaondoa mashabiki wa Simba vichwa chini huku Yanga wakishangilia kwa kukebehi: Okwi, Okwi, Okwi.

Beki wa zamani wa Simba, Derrick Walulya, jana alionekana kulipa kisasi cha kutemwa na timu hiyo katika kipindi hiki cha usajili, baada ya kumdhibiti vilivyo Felix Sunzu na kumfanya ashindwe kufurukuta kabisa.

Alikuwa akipanda na kushuka akionyesha kiwango maridadi kabisa.

Katika dakika ya 38, URA walionyesha kukifunika vilivyo kikosi cha Simba baada ya kupiga pasi 29 ambazo wanaodhaniwa kuwa ni mashabiki wa Yanga walikuwa wakizihesabu kwa sauti kubwa.

Baada ya mchezo huo, Milovan alikiri: “Tumecheza na timu ngumu, tulianza vizuri kipindi cha kwanza lakini cha pili hatukucheza vizuri, nampongeza Walullya kwa kuonyesha kiwango kizuri, nimeshangaa kuona hivyo.”

Katika mchezo wa awali uliopigwa saa 8:00 mchana kwenye uwanja huo, Vita Club ya DR Congo iliishindilia Ports ya Djibouti mabao 7-0, wakati kule Chamazi mechi ya Azam dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa Yanga kuvaana na Wau Salaam ya Sudan Kusini kwenye Uwanja wa Taifa huku APR ya Rwanda ikionyeshana kazi na Atletico ya Burundi katika mechi ya awali kwenye uwanja huo.

No comments:

Translate