WATANZANIA
 tumekumbwa tena na balaa la ajali  kubwa ya meli kuzama. Ni wakati sasa
 wa kujifunza kutokana na yaliyotokea huko nyuma.
Maana
 ajali ya Mv Skagit  inaonekana dhahiri kuchangiwa na uzembe. Na uzembe 
kwa nchi yetu unalelewa na mfumo mbovu. Na mfumo mbovu unatokana na 
Katiba mbovu.
Maana,
 ni katika mazingira haya ya kufanya mambo ya hovyohovyo ndipo 
tunapokuwa na  wanasiasa wa hovyohovyo wenye  kuhusika pia na biashara 
ya uchukuzi na usafirishaji wa abiria.  
Ni
 vigumu kwa mfumo wetu wa sasa, kwa watendaji wa vyombo au taasisi 
zisizo huru kikatiba na kisheria kuweza kuwasimamia wafanyabiashara 
dhalimu ambao miongoni mwao wamo baadhi ya wanasiasa wetu.
Tuna
 lazima sasa kupitia Katiba yetu ijayo, kuvipa nguvu za kisheria vyombo 
na taasisi zetu muhimu kwa nchi yetu. Tuwe na vyombo na taasisi huru 
ambazo utendaji wake hauwezi kuingiliwa kirahisi na mamlaka nyingine.
Fikiri
 leo kama tungekuwa na utaratibu wa kwamba mmiliki wa chombo cha majini 
au angani na atakayebainika kuingiza nchini chombo kilicho chini ya 
viwango vinavyokubalika kimataifa na hata  chombo hicho kikasababisha 
ajali ya kuua raia kuwa mmiliki huyo atafungwa jela na kufilisiwa mali 
zake? Naamini, tungekuwa na vyombo madhubuti na ajali zingetokea kwa 
bahati mbaya kwa maana yake halisi.
Ni nini basi cha kujifunza kutoka kwenye ajali iliyopita ya Mv Spice Islanders?
Ikumbukwe,
 Ripoti ya Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv Spice 
Islanders ilipendekeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Mustafa 
Aboud Jumbe pamoja na wahusika wengine wachukuliwe hatua za kisheria na 
kinidhamu kutokana na uzembe waliofanya na kusababisha kuzama kwa Meli 
hiyo. Mpaka leo hii hatujasikia adhabu walizopewa wahusika wa ajali ile.
Maana,
 bado tunakumbuka kuwa, ripoti ile ilibainisha kuwa miongoni mwa watu 
ambao walibainika na makosa katika ajali ya Mv Spice Islanders ni pamoja
 na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar, Haji Vuai 
Ussi, Mkuu wa kituo cha usimamizi wa  usalama wa vyombo vya baharini wa 
Shirika la Bandari, Usawa Khamis Said na Kaimu Mdhibiti wa Bandari ya 
Malindi, Sarboko Makarani Sarboko.
Wengine
 ni pamoja na Wanahisa wa Kampuni inayomiliki meli hiyo Jaku Hashim Ayub
 ambaye ni Mwakilishi na Mbuge wa Jimbo la Muyuni, Salim Said Mohammed, 
 Makame Hasnuu Makame na Yussuf Suleiman Issa.
Alikuwamo
 pia nahodha  wa meli  Said Abdallah Kinyanyite na wasaidizi wake, Ofisa
 usafirishaji wa Shirika la Bandari Hassan Mussa Mwinyi na Mkaguzi wa 
Meli wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini, Juma Seif Juma.
Ndiyo, wakati bado hatuna hakika ya hatua zipi zilichukuliwa dhidi ya wahusika hawa leo tunaomboleza msiba mwingine kwa taifa.  
Hakika,
 inasikitisha sana, kuwa hata mwaka haujatimu kukumbuka ajali iliyopita 
ya Septemba 9, 2011, Watanzania tunapatwa na msiba mwingine. Na misiba 
yote miwili inatokana na uzembe na wala si ya kusingizia ‘Kazi ya 
Mungu’.
Watanzania
 sasa tunataka kuona hatua kali za kisheria na kinidhamu zinachukuliwa, 
tena kwa haraka dhidi ya wahusika waliochangia kwenye ajali ile ya Mv 
Skagit.
Kwa
 kuanzia jina la mmiliki wa meli liwekwe hadharani. Na Tume 
itakayochunguza ajali hii itabaini kuwa mwenye meli  ameingiza chombo 
chakavu, basi, awe wa kwanza kutolewa mfano.

 
No comments:
Post a Comment