MTAALAMU WA ATOMIKI ASIMULIA ALIVYOELEA BAHARINI KWA SAA NNE BILA KUJUA KUOGOLEA
Waandishi Wetu
WAKATI
jitihada za kuopoa miili ya watu waliofariki dunia katika ajali ya meli
ya MV Skagit iliyozama Jumatano wiki hii zikiendelea, walionusurika
kwenye ajali hiyo wameeleza jinsi walivyokumbana na zahama, mmoja wao
akiwa mkazi wa Micheweni Pemba, Makame Masoud Ali (18), ambaye alisema
kilichomsaidia hadi alipookolewa ni kushikilia gunia kwa zaidi ya saa
mbili akielea nalo baharini.
Mbali na Ali, mwingine ni mfanyakazi
wa Tume ya Nguvu za Atomiki Arusha, Salome Mwambinge ambaye alisema:
“Kuokoka kwangu ni miujiza ya Mungu.”
Mwambinge ambaye amelazwa
katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar alisema: “Sijui kuogelea,
lakini nilikaa kwenye maji kwa saa nne. Nilichoka na kukakata tamaa,
nikajiachia ili ikiwezekana nife, lakini nashangaa leo hii ni mzima.”
Mtumishi
huyo Tume ya Atomiki ambaye alikuwa safarini kuelekea Pemba kikazi,
alisema aliokolewa akiwa hajitambui... “Ninachokumbuka ni kwamba
waokoaji walinifunga kamba shingoni nikapata maumivu makali, nikapiga
kelele wakaniachia, nikatumbukia tena kwenye maji na baadaye
walifanikiwa kuniokoa na kuniweka kwenye boti.”
Alisema wakati akiwa katika harakati za kujiokoa, aliwaona watu kadhaa wakiwa wamekufa wakiwamo watoto.
Kwa
upande wake, Ali alisema baada ya meli kuzama na yeye kutupwa nje,
aliona gunia na kulidaka. Anasema alilishikilia kwa zaidi ya saa mbili
kabla ya kuonwa na vikosi vya uokoaji.
Abiria mwingine mkazi wa
Bagamoyo, Hamisa Akida alisema meli hiyo ilizama ghafla na haikuwa
rahisi kuwa na maandalizi ya kujiokoa: “Kwa jinsi meli hiyo ilivyozama
ghafla haikuwa rahisi kujiokoa, kilichotokea hadi tukaokolewa ni mapenzi
ya Mungu,” alisema.
Alisema hali alipookolewa alikuwa ameshakunywa maji mengi na kuishiwa nguvu... “ lakini nashukuru ni mzima.”
Waliopatikana jana
Wakati
majeruhi hao wakieleza hayo, jitihada za vikosi vya uokoaji hadi jana
zilifanikisha kupatikana kwa miili 68 na kati ya hiyo 16 ilitambuliwa.
Waliotambuliwa ni Husna Ali Hamis (34) na
Kulthum Haji Khamis (34) wote wakazi wa Bagamoyo na Sichana Pandu (45 wa Kilimahewa Zanzibar).
Wengine
ni Nadra Maulid Mkubwa (17) wa Chumuni, Zanzibar, Mwanaidi Abdallah
Ramadhani (21) wa Morogoro, Zubeda Jumanne Kwagaya (26- Meya),
Idd
Masoud Omari (Miezi 7- Tomondo) Riziki Mohamed Idd (21- Fuoni
Zanzibar), Mwanaisha Khamis Haji (75) na Amina Shabani Kibega (24) wote
wa Jang’ombe, Zanzibar.
Pia wamo Laki Victor Kadoro (28- Mbagala, Dar es Salaam), Damas Leo Mlima (54- Shangani),
Halima Sharifu Abdala (21-Kigamboni, Dar es Salaam), Ali Juma Ali (44- Jang’ombe, Zanzibar),
Raya Ramadhani Hasani (2- Shakani) Mwanaisha Omari Juma (20- Bunju, Dar es Salaam) na Maryam Idd Omari Omari (25) Shakani.
Washindwa kutambua miili
Hali
katika Viwanja vya Maisara, wanakohifadhiwa maiti jana kulikuwa na
mkanganyiko baada ya wananchi wengi kushindwa kuwaona ndugu zao ambao
walikuwa wamesafiri katika meli hiyo wakiwamo raia wa kigeni.
Maiti
moja ya raia wa Kenya imetambuliwa na ndugu zao ambao hata hivyo,
walisema wamechanganyikiwa kuhusu namna ya kusafirisha mwili kwenda
kwao.
Mmoja wa ndugu, John Mumee alisema wameitambua maiti ya
ndugu yao aitwaye Martina Masela... “Lakini hatujui tutaisafirisha vipi
kwenda Mombasa kwa sababu hatuna fedha, lakini pia hatuelewi
tutasafirisha kwa njia gani kwa sababu mashirika ya ndege hayataki
kusafirisha maiti.”
Alisema marehemu alikuwa akisafiri na mumewe,
Bernard Kalii kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar wakiwa na ndugu
mwingine, Mary Kioko ambao bado hawajapatikana.
“Tumepata maiti
hiyo moja lakini wenzake wawili bado hatujawapata, hatuelewi tufanye
nini hapa tumechanganyikiwa tunaomba msaada wa haraka,” alisema Mumee.
Waliiomba
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwasiliana na Ubalozi wa Kenya
nchini ili kuona kama kuna uwezekano wa kuwasaidia kuisafirisha maiti
hiyo ambayo alisema imeanza kuharibika.
Mkazi wa Temeke, Dar es
Salaam, Ali Mzee Moto alisema, hadi sasa hajawaona binti yake, Mwamini
Ali aliyekuwa na mtoto wake mchanga.
“Walisafiri na meli hiyo na
walikuwa wakipitia Zanzibar ili siku inayofuata waende Pemba. Alikuwa
anamfuata mchumba wake lakini Mungu hakupenda afike huko,” alisema Moto.
Alishangazwa na shughuli ya uokoaji kusuasua na kuhoji sababu za Serikali kushindwa kuomba msaada wa waokoaji kutoka nje.
“Tunafahamu ndugu zetu watakuwa wamekufa, lakini tunachoomba sisi ni kupata miili yao ili twende tukawazike,” alisema Moto.
Mwingine
aliyepotelewa na mtoto ni Philip Cassian John anayefanya kazi Trans
Cargo, Dar es Salaam alisema, hajamwona mwanaye Thobias Joseph,
anayefanya kazi katika Kampuni ya Hugo Domingo aliyesafiri na meli hiyo
kwa safari za kikazi.
“Walisafiri na wafanyakazi wenzake ambao
maiti zao zimepatikana, sasa niko hapa kusubiri kati ya watakaookolewa
leo kama nitamwona mwanangu.”
Maiti zaharibika
Kati
ya maiti 68 zilizoopolewa baharini, 10 hazikutambuliwa na zilizikwa
jana na SMZ katika makaburi ya Kama huko Bububu, Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia mazishi, Abdallah Twalib alisema maiti zimeharibika vibaya.
“Hata
baadhi ya ndugu waliozitambua maiti zao wameiomba Serikali izike kwenye
makaburi ya eneo la Kama baada ya kuharibika vibaya,” alisema.
Sijiuzulu ng’o
Juzi,
Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad
alisema hawezi kujiuzulu kwa tukio hilo kwa kuwa ni mapenzi ya Mungu.
Hamad
alisema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa na mawaziri
wenzake wanne kutoka katika Serikali ya Muungano na wa SMZ. Hao walikuwa
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu, Waziri wa Habari na Michezo wa SMZ, Ali
Mbarouk na Waziri wa Katiba na Sheria SMZ, Aboubakar Hamis.
Alipoulizwa
kama ana mpango wa kujiuzulu kutokana na ajali hiyo ambayo ni ya pili
kutokea katika kipindi cha mwaka mmoja, Hamad alisema: “Hivi ningezuiaje
upepo usitokee?
Ajali hii ni mapenzi ya Mungu kwani haiwezi
kuzuiliwa na binadamu kwa sababu imetokana na upepo mkali na ilitokea
ghafla, katika kipindi kisichozidi dakika tano meli ilikuwa imezama,”
alisema Hamad.
“Kujiuzulu siyo utatuzi wa tatizo, bali ni kumwomba Mungu atuepushe na majanga kama haya ambayo hayawezi kuzuiwa na binadamu.”
Waziri
huyo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa anayetokea Chama cha CUF alisema,
kauli za kumtaka ajiuzulu ni mbinu chafu za kisiasa zinazofanywa dhidi
yake ili aonekane hafai kuongoza.
“Walinipiga vita hata kwenye
ajali ya meli ya Mv Spice Islander wakitaka nijiuzulu lakini hata majibu
ya tume iliyoundwa kuchunguza ilinisafisha kwamba sihusiki,” alisema.
Dk
Mwakyembe alisema Watanzania hawana sababu ya kumtafuta mchawi wa ajali
hiyo kwani imetokea kwa bahati mbaya... “Tukubali kwamba ajali hii ni
bahati mbaya. Maofisa wetu wametuthibitishia bila kuwa na shaka kwamba
meli ilikuwa nzima na haikuzidisha abiria, kujiuzulu siyo suluhisho,
tushikamane katika kipindi hiki kigumu.”
Uzoefu wa mabaharia
Mmoja wa mabaharia katika Kivuko cha Bandari ya Dar es Salaam, John Peter amesema Serikali inapaswa kulaumiwa kwa tukio hilo.
Peter
ambaye amekuwa baharia kwa miaka 24 sasa alisema, pamoja na Serikali
kuwa na wataalamu wa kukagua vyombo hivyo kabla, ufisadi katika usajili
wa meli bado ni tatizo.
“Kama Marine Suveyer (Mtafiti wa Meli) angetekeleza majukumu yake, naamini tusingekuwa na meli mbovu kama hizi,” alisema.
Baharia
mwingine mwenye uzoefu wa miaka 40, maarufu kama Kepteni Magamba
alisema anayepaswa kulaumiwa katika ajali hiyo ni kiongozi wa safari za
meli.
Kiongozi huyo (Port State Controller) hupokea taarifa kutoka
mamlaka ya hali ya hewa na kuruhusu meli iondoke au isiondoke. Kiongozi
huyo husimamia usalama wa meli ndani na nje ya bahari kwa kushirikiana
na eneo meli inapoelekea.
“Meli kabla ya kuondoka lazima ifuate
taratibu zote, nahodha hupata kibali kutoka Sumatra (clearance) na
kuipeleka kwa ‘Port State Controller’ ambaye tayari anakuwa ameshapata
taarifa za hali ya hewa,” alisema Magamba.
Wanasiasa
Vyama
kadhaa vya siasa vimetoa salamu za pole kwa wafiwa na kuishauri
Serikali kuongeza umakini katika ukaguzi wa vyombo vya baharini.
Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliitaka Serikali kuangalia upya
uwajibikaji, utendaji na mwenendo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa
Nchi Kavu na Majini (Sumatra) akidai kuwa taasisi hiyo imeshindwa
kuwajibika ipasavyo kudhibiti vyombo vya usafiri.
Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willbrod Slaa ameshauri kanuni za Bunge zinazotumika hivi
sasa kuangaliwa upya ili kuruhusu Bunge kujadili ajali hiyo...
“Nimesikitishwa na kitendo cha Naibu Spika (Job Ndugai) kuzuia wabunge
kujadili suala la kuzama kwa meli bungeni kwa maelezo kuwa kanuni
haziruhusu. Nitoe wito kwa kanuni kuangaliwa upya ili kuruhusu Bunge
kujadili masuala ya kitaifa pindi yanapotokea.”
Mwenyekiti wa APPT
Maendeleo, Peter Mziray alisema: “Lipo tatizo katika uingizaji, ukaguzi
na usajili wa vyombo vya usafirishaji wa majini… Serikali na mamlaka
zinazohusika na usajili hazifanyi kazi kwa kuzingatia umuhimu wa kazi
waliyopewa na matokeo yake ndiyo kuruhusu vyombo vibovu kubeba roho za
watu.”
Sumatra yajitetea
Hata hivyo, Sumatra
imejitetea kwamba haitambui usajili wa boti hiyo ya Mv Skagit. Meneja
Uhusiano wa Sumatra, David Mziray alisema meli hiyo ilisajiliwa na
Mamlaka ya Usafiri wa Majini Zanzibar (ZMA).
Alisema meli hiyo
ilipewa cheti cha ubora na mamlaka hiyo Agosti, 24 mwaka jana ambacho
kinamalizika muda wake, Agosti 23, mwaka huu ikiwa na uwezo wa kubeba
abiria 300 na tani 26 za mizigo... “Hatuwezi kutoa maelezo zaidi kwa
sababu ilisajiliwa Zanzibar na si huku kwetu.”
No comments:
Post a Comment