tangazo

Friday, July 6, 2012

KAMPENI ZA UCHAGUZI YANGA ZAFUNGULIWA RASMI

                     


PAZIA la kampeni za uchaguzi wa uongozi katika klabu ya Yanga linafunguliwa leo kwa wagombea wote kuanza kampeni zao tayari kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Julai 15.Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, Francis Kaswahili alisema jana kuwa wagombea wote tayari wameshawasilisha vyeti vyao.

"Wagombea wote hawana matatizo, wameshawasilisha vyeti vyao na nimeshavipeleka TFF, kampeni rasmi zinaanza kesho (leo),"alisema Kaswahili.

Uchaguzi wa Yanga umekuja baada ya kujiuzulu kwa wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji wakiongozwa na Mwenyekiti wao Lloyd Nchunga kutokana na shinikizo la wanachama wakiongozwa na Baraza la Wazee.

Uchaguzi huo ni uchaguzi mdogo na watakaoingia madarakani wataitumikia klabu hiyo kwa miaka miwili iliyosalia kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.

Kampeni hizo zitadumu kwa muda wa siku tisa kwa wagombea kunadi sera zao kwenye matawi zaidi ya 100 ya klabu hiyo yenye wanachama zaidi ya 4 milioni.Uchaguzi huo ambao umedhaminiwa na TBL kwa Sh 20 milioni umepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Nafasi zitakazowaniwa ni ile ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.Tayari wanachama mbali mbali wameunda makundi yao ya kuyapigia debe ili kushinda katika kinyang'anyiro hicho, ambapo mchuano mkali upo kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti inayowaniwa na Clement Sanga na Yono Kevela.

Pia mchuano mkali upo pia katika wanaowania nafasi za wajumbe, ambapo yupo Abdallah Bin Klebu, Edgar Fongo, Haron Nyanda, Omary Ndula, Saleh Abdallah, Jumanne Mwamenywa, Abdallah Sharia, Peter Haule, Musa Katabalo, Lameck Nyambaya, Ramadhani Kampira, Ramadhani Said, Beda Tindwa, Mohamed Gayo Justine Baruti na Jamali Kisongo.

No comments:

Translate