Tukio la kutekwa na ‘kusulubiwa’ kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka hivi karibuni, limeibua mambo mazito, Risasi Jumamosi limedaka ishu nyeti.
KUNA KUNDI LA MAFIA?
Habari zinazozungumzwa mitaani juu ya tukio hilo ni nyingi lakini mpya ni madai kuwa kuna kundi la watu limeundwa linalojishughulisha na ‘umafia’ wa watu tishio wenye ushawishi katika jamii wanaohamasisha migomo na kukosoa serikali waziwazi.
Imeenea kuwa kundi hilo halina uhusiano na serikali wala chama chochote cha kisiasa nchini kama baadhi ya watu wanavyodai na tayari Rais Jakaya Mrisho Kikwete alishakanusha utawala wake kuhusika na jambo hilo baya.
“Ukweli ni kwamba kuna kundi ambalo kazi yake ni kufanikisha matukio kama hili la Dk. Ulimboka ili kuifanya serikali ishindwe kutawala,” chanzo kiliweka wazi.
Hata hivyo, mwandishi wetu alipodadisi faida ambazo kundi hilo litapata baada ya kufanikisha mpango huo wa kutikisa amani ya nchi kwa kuwafanyia umafia watu wanaoikosoa serikali, chanzo kilidai kwamba ni kutimiza lengo la kuwafanya watu waichukie serikali iliyopo madarakani ili utawala mwingine upate nafasi ya kutawala nchi na kulipa kundi hilo heshima.
“Unajua kundi hilo litakuwa linawadhuru watu ambao wanafahamika kwa kuchochea migomo au kuikosoa serikali ili raia wadhani anayefanya hivyo ni serikali kwa hiyo waichukie, ipoteze mvuto kwa jamii na kundi hilo nalo liweze kufaidi rasilimali za taifa,” chanzo kilisema.
KUBENEA NA NDIMARA
Ukimwondoa Dk. Ulimboka, wengine ambao waliwahi kuonja matunda ya umafia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers, inayochapisha Gazeti la Mwanahalisi, Saed
Kubenea na Mhariri Mshauri wa gazeti hilo, Ndimara Tegambwage.
Wanahabari hawa, mapema mwaka 2008 walivamiwa ofisini kwao zilizopo Mtaa wa Kasaba,
Kinondoni, Dar na kufanyiwa ukatili na watu wasiojulikana.
Katika tukio hilo, Kubenea alimwagiwa tindikali na Ndimara kukatwakatwa na mapanga - gazeti lao linahusishwa na ukosoaji wa serikali waziwazi.
MWAKYEMBE
Mwingine ambaye aliwahi kudaiwa kukutana na umafia na kusababisha kuharibika kwa ngozi ni Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe huku ulipuaji wake wa ile skendo ya Richmond ukitajwa kumponza.
MUKOBA NA MGAYA
Habari zilidai kuwa watu wengine ambao jamii inawaombea kwa Mungu wasikutane na umafia huo ni pamoja na Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali (TUCTA), Ernest Mgaya.
ZITTO NA MNYIKA
Wengine wanaolindwa na raia kwa maombi ni wabunge vijana wa Chadema ambao ni wakali hasa linapokuja suala la maslahi ya taifa, Zitto Kabwe wa Kigoma Kaskazini na John Mnyika wa Ubungo ambaye hivi karibuni alitolewa nje ya bunge kwa kuvunja kanuni.
GODBLESS LEMA
Huyu kwa sasa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema ambaye alivuliwa ubunge wa Arusha Mjini baada ya kushindwa kesi mahakamani lakini amekuwa akizunguka nchini kuhamasisha mabadiliko, huku akiikosoa serikali majukwaani hivyo kujiweka katika wakati mgumu wa kumfika ya Dk. Ulimboka.
TURUDI KWA DK. ULIMBOKA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesisitiza kuwa, jopo la upelelezi aliloteua kushughulikia tukio zima la kutekwa kwa Dk. Ulimboka litaendelea na kazi yake hadi mwisho na hatasikiliza kelele za wanaodai kutokuwa na imani nalo.
UHAKIKA DK. ULIMBOKA ANATIBIWA UJERUMANI
Baada ya kuwepo kwa utata wa nchi ambayo Dk. Ulimboka alipelekwa kutibiwa, Risasi Jumamosi lilipekuwa vyanzo vyake na kuthibitishiwa kuwa baada ya hali kuwa mbaya daktari huyo amehamishiwa nchini Ujerumani kwa matibabu zaidi.
MH! MAJIRANI HUWA WANAMUONA TU KWENYE ‘MIDIA’
Kwa mujibu wa majirani waliozungumza na gazeti hili mtaani kwake anapoishi Mbezi ya Kimara, Dar walisema kuwa, wamezoea kumuona Dk. Ulimboka kwenye vyombo vya habari ‘midia’ lakini mtaani kwake amekuwa nadra kupatikana.
No comments:
Post a Comment