suleiman kova
RAIA
wa Kenya, Joshua Mulundi (21) amekamatwa na polisi jijini Dar es
Salaam na kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumteka na kufanya
jaribio la kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk Steven
Ulimboka.Mtuhumiwa huyo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jana alasiri na kusomewa mashtaka mawili na Wakili
wa Serikali, Ladslaus Komanya.
Wakili
Komanya alidai mahakamani hapo kuwa Mulundi ambaye makazi yake ni
Murang'a nchini Kenya kuwa, mnamo Juni 26, mwaka huu akiwa eneo la
Leaders Club, jijini Dar es Salaam alimteka Dk Ulimboka.
Hata
hivyo, kumetokea utata wa jina, umri wake na makazi ya mtuhumiwa huyo,
kwani wakati hati ya mashtaka mahakamani inasema ni Joshua Mulundi
mwenye umri wa miaka 21 na mkazi wa Murang’a nchini Kenya, taarifa ya
Jeshi la Polisi imesema anaitwa Joshua Mahindi mwenye miaka 31 na mkazi
wa Namanga nchini Kenya.
Katika
shtaka la pili, Wakili Komanya alidai kuwa tarehe hiyohiyo mshtakiwa
alifanya jaribio la kumsababishia kifo Dk Ulimboka kwa kumpiga katika
eneo la Msitu wa Pande eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam, kinyume cha
sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo akidai kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo siyo sahihi.
Hakimu
Mkazi, Agnes Mchome alimwambia kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, isipokuwa
Mahakama Kuu pekee.
Siku ambayo Dr Ulimboka akipelekwa Hospitali baada ya kupigwa.
Hakimu Mchome aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 5,2012 itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Taarifa ya Polisi
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi mshtakiwa huyo anajulikana kwa jina la Joshua Muhindi (31), mkazi wa Namanga nchini Kenya.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP)
Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mshtakiwa huyo
alikamatwa Juni 29 mwaka huu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko
Kawe baada ya taarifa kutoka kwa wasamaria wema.
Alisema
raia huyo mwenye kitambulisho cha utaifa namba 29166938 kilichotolewa
Oktoba 11, 2010 katika Wilaya ya Nyeri nchini Kenya, pia anamiliki hati
ya dharura ya kusafiria yenye namba 0123431 iliyotolewa Juni 14, mwaka
huu Namanga Kenya.
Kwa
mujibu wa Kova, baada ya kuhojiwa na polisi, raia huyo alisema alikuja
nchini Juni 23, mwaka huu kwa ajili ya kufanya tukio lililotokea Juni
25 mwaka huu na kwamba alijulishwa kuwa yeye na wenzake 12 ndiyo
walipangwa kutekeleza tukio hilo.
Alisema
raia huyo na wenzake walikuja nchini kwa ajili ya kumdhuru Dk
Ulimboka, baada ya kukodiwa na mtu ambaye hakumtaja jina ambaye
anaamini ni mtumishi wa Serikali.
“Baada
ya kuhojiwa alidai kuwa yeye ndiye aliyehusika kumteka Dk Ulimboka na
wenzake na baada ya utekaji huo wenzake waliondoka,” alisema Kova na
kuongeza:
“Alisema
walikuja kutekeleza tukio hilo kwa lengo la kujua ni nani
anayemshawishi Dk Ulimboka na alipelekwa na mwenyeji wake asiyemtambua
hadi katika hoteli moja katikati ya jiji.”
Alisema
mtuhumiwa huyo na wenzake 12 wako kwenye kikundi kijulikanacho kama
Gun Star chenye makao yake Iwiru Wilaya ya Thika nchini Kenya na kwamba
kinaongozwa na mtu mmoja ajulikanaye kama Silencer akisaidiwa na Paft.
Alisema
pia, mtuhumiwa huyo alidai kuwa, wamekuwa wakijihusisha na matumizi ya
silaha na kwamba wamekuwa wakifanya matukio mengi ya kihalifu nchini
Kenya.
Alisema
baada ya utekaji huo, Juni 29 mwaka huu raia huyo alikwenda katika
Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe kwa nia ya kutaka kuonana na
kiongozi wa kanisa hilo Mchungaji Gwajima, lakini hakufanikiwa badala
yake alionana na msaidizi wake ajulikanaye kama Joseph Marwa Kiriba.
“Alipoonana
naye alimweleza kuwa yeye ni mwanachama wa Kikundi cha ‘Umafia’ na
kwamba hukodiwa kufanya matukio ya kihalifu Kenya na nje ya mipaka,”
Kamanda Kova alisema.
“Alikwenda
katika kanisa hilo kwa ajili ya kufanya toba maana aliona alifanya
kitendo cha kinyama hivyo aliona arudi ili akapate toba,” alisema.
Alisema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi kwa ajili ya kuwatafuta watu wengine waliohusika na utekaji huo.
Katika
hatua nyingine, jeshi hilo pia limewakamata watu wanane ambao
wanadaiwa kuhusika na uvamizi wa mashamba katika eneo la Kawe.
Maandamano ya madaktari yazuia
Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limepiga marufuku maandamano
ya madaktari yaliyopangwa kufanyika Jumatatu ijayo kushinikiza mambo
kadhaa ikiwamo kuundwa tume huru ya kuchunguza kutekwa, kuteswa na
kutupwa katika Msitu wa Pande kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari
Tanzania, Dk Steven Ulimboka.
Kamanda
wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleman Kova aliwaambia waandishi wa habari
jana kuwa maandamano hayo hayatafanyika kutokana na sababu mbalimbali
zikiwamo za kiusalama.
Alisema wamesitisha maandamano hayo kwa sababu madai ya madaktari tayari yameshashughulikiwa na Serikali.
“Tumesitisha
maandamano kwa sababu tunahofia kunaweza kutokea uvunjifu wa amani
maana Waislamu nao walipanga kuandamana kesho (leo),” alisema Kova.
Msimamo wa madaktari
Kauli
hiyo ya Kova ilitolewa saa chache baada ya kikao cha zaidi ya
madaktari 400 waliokutana katika mkutano wa dharura ulioitishwa na
Chama cha Madaktari (MAT), ambako waliridhia kufanyika kwa maandamano
hayo.
Katibu
wa (MAT) Dk Rodrick Kabangila alisema katika kikao hicho, madaktari
hao walipokea taarifa ya MAT iliyoeleza hatua zilizochukuliwa na
Serikali dhidi ya wenzao waliofukuzwa.
“Madaktari
wamepokea taarifa za wenzao kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji, ikiwamo
kufukuzwa katika makazi yao kwa kutumia Polisi wa Kutuliza Ghasia
(FFU), kunyimwa chakula, posho na kuelezea kuwa vitendo hivyo ni vya
unyanyasaji na uonevu dhidi ya taalamu na udaktari wenyewe,” alisema Dk
Kabangila.
Dk
Kabangila alisema kuwa, kufuatia hatua hiyo madaktari hao wamepitisha
azimio la kufanya maandamano ya amani ambayo yanatarajia kushirikisha
madaktari zaidi ya 800 hadi 1,000 na kutoa wito kwa wananchi wenye
mapenzi mema na taaluma hiyo, kushiriki wakiwa na vitambaa vyeupe.
Akizungumzia
msimamo wa polisi kuyazuia maandamano hayo, Dk Kabangila alisema
uongozi wa madaktari utakutana kujadili tamko hilo la polisi.
“Tumepata
barua inayozuia maandamano yetu. Barua hii imetoa sababu ambazo ni
tofauti na sisi tulichoomba. Sisi (MAT) ndio tulioomba maandamano kwa
ajili ya kuonyesha hisia zetu juu ya vitendo wanavyofanyiwa madaktari,”
alisema Dk Kabangila.
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment