MASHABIKI wa Simba jana waligeuka 'mbogo' kwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' wakitaka kujua ukweli kuhusiana na tetesi za mshambuliaji wao tegemeo, Emmanuel Okwi kujiunga na Yanga.
Mashabiki hao waliojitokeza kwa wingi makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi walimzonga Kaburu wakati anatoka kwenye mkutano na vyombo vya habari kukanusha taarifa za Okwi kwenda Yanga.
Kaburu aliwatoa hofu mashabiki hao kwa kuwaambia Okwi bado ni mchezaji wao na wasiwe na wasiwasi na kuingia kwenye gari yake aina ya Noah na kufunga vioo na kuondoka.
Kitendo hicho kiliwafanya mashabiki hao kutoa maneno ya vitisho kwa kiongozi huyo kwa kudai hawatakubali kuona Okwi anakwenda Jangwani bila ya maelezo ya maana kutoka kwa viongozi wao wa Simba.
"Kaburu usituzingue kabisa, Yondani (Kelvin) mlituambia hivyo hivyo, tunakwambia kabisa kama Okwi atacheza Yanga hapatatosha hapa," alisikika shabiki mmoja akiongea kwa hasira.
Awali akizungumza na Wanahabari, Kaburu alisema mkataba wa Okwi utamalizika mwakani mwezi Juni na hivi sasa Okwi yupo nyumbani kwao Uganda akijianda kwa safari yake ya kwenda Italia kwa majaribio keshokutwa.
Kaburu alionyesha mkataba aliosaini Okwi wa kuichezea Simba mwezi Novemba mwaka jana ambao unaonyesha mkataba huo utalimalizika Juni 13 mwaka ujao.
"Okwi sasa hivi yuko kwao Uganda anakamilisha suala la viza ya kwenda nchini Italia kwenye majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Parma Fc,"alisema Kaburu.
Hata hivyo; Kaburu alikwenda mbali zaidi baada ya kumpigia simu mchezaji huyo na kumuunganisha na waandishi wa habari, ambapo alikiri kuwa hana ndoto za kuichezea Yanga na akili yake ameielekeza Ulaya.
" Viza yangu inatoka leo (jana), siku mbili zijazo naenda Italia, akili yangu nimeelekeza kucheza professional (soka ya kulipwa) na kama nitabaki basi nitacheza Simba kwa sababu bado nina mkataba nao," alisema Okwi kwa kifupi kwa njia ya simu.
Sakata hilo limeibuka baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kuwa mchezaji huyo amemwaga wino wa kuichezea Yanga msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Pia, Kaburu alisema iwapo kweli Yanga wanamtaka mchezaji huyo basi wafuate kanuni kwa kukaa meza moja na uongozi kwa kuwa moja ya kipengele katika mikataba yao kwa baadhi ya wachezaji akiwamo Okwi na Yondani ni kuwa haiwaruhusu kufanya mazungumzo na klabu yoyote ya ndani hususani Yanga isipokuwa klabu za nje ya nchi.
Kaburu alisema kuna uwezekano mkubwa mchezaji huyo akacheza Italia ingawa pia ana mpango wa kwenda kwenye majaribio nchini Ujerumani, huku timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns za Afrika Kusini zikionyesha nia ya kumtaka nyota huyo.
Katika hatua nyingine, Kaburu alisema tayari beki Juma Nyoso amesaini mkataba wa mwaka mmoja tangu Julai Mosi wa kuendelea kubaki Simba.
Pia alisema wamefikisha barua yao kwa Shirikisho la Soka Tanzania juu ya kitendo cha Yanga kumsajili Kelvin Yondani kinyume na taratibu.
"Desemba 23 tuliingia mkataba na Yondani, tumeshangazwa kusikia amesaini Yanga na anaonekana anafanya mazoezi huko, tumeshamuita kwenye mazoezi yetu na suala hili tumeshaliripoti TFF, tunasikitika mpaka leo hii TFF hawajatujibu barua yetu,"alisema Kaburu.
Alisema,"sisi tunafuata sheria, Yondani hataichezea Yanga, wakitaka Yanga waje tukae meza moja, tumeshawambia wazi huyo mchezaji wanayemng'ang'ania atawagharimu."
No comments:
Post a Comment