Baba mzazi wa Diamond(Abdull Juma)
Naseeb Abdull(Diamond)
SIKU
chache baada ya kuibuka kwa baba aliyemlea Nasibu Abdul ‘Diamond
Platinumz’ aitwaye Abdul Juma na kudai kuwa mwanaye huyo amemtelekeza na
hamjali, mwanamuziki huyo amemchana mzazi wake huyo, Ijumaa lina kitu
kamili.
Akizungumza redioni kupitia Clouds FM, Jumatatu wiki hii,
Diamond alidai kushangazwa na mzazi wake huyo huku akimtaka kuacha
kusema maneno hayo kwani siyo mazuri.
Huyu hapa Diamond ambaye kwa sasa yupo juu kuliko msanii yeyote Bongo kimuziki:
“Kiukweli
ni vitu ambavyo mimi vimenishangaza sana kwa sababu sijui chochote na
nisingependa nisikie suala la mzazi wangu kusema mimi ni mtoto wake,
sijui nini na nini kwamba mimi nafanya starehe sihusiki na yeye, siyo
kauli nzuri kiukweli, ina maana ananijua kwamba mimi ni mwanaye baada ya
kuwa Diamond?
“Siku zote kama alijua mimi ni mtoto wake, basi
angenisomesha na kunipa elimu nzuri, lakini nilihangaika na mama yangu
mzazi (Sanura Khassim ‘Sandra’) akanikuza na kunisomesha kwa shida na
tabu zote mpaka leo nimekuwa hivi nilivyo, nisingependa kumsikia mtu
yeyote anaongea kwamba mimi ni mtoto wake au yeye ni nani kwa sababu
siku zote hawakuonekana, wasitake kuonekana kipindi cha masilahi, mtu
ndiyo anajifanya anahusika sana na mimi kama mtoto wake.
“Haya mambo
nilianza kuyasema toka nilipotoa single (wimbo) ya Binadamu, sikujua
hata kama leo ningekuja kuwa na Prado (gari alilonunua juzikati la zaidi
ya Sh. milioni 60), makazi (anajenga nyumba Tegeta, Dar na tayari
imetumika Sh. milioni 69) au kuwa na haya mafanikio mengine, baba yangu
ataendelea kuwa baba yangu tu ila siwezi kumpa kipaumbele kama
ninachompa mama yangu kwa sababu kama angetaka hilo angenijali toka
mapema.
“Mimi nilikuwa napenda kusoma na nilikuwa nafanya vizuri
kwenye masomo yangu, lakini sikuwa na uwezo wa kifedha kuendelea kusoma,
mzazi wangu alikuwa na fedha, ina maana angenijua mimi angenisomesha,
leo ningekuja kuwa hata mbunge au waziri kwa sababu mimi najua nina upeo
mkubwa sana wa kielimu na vitu vingine, sasa nimesota na muziki halafu
leo ndiyo wanajitokeza.
“Sitaki, naomba waniache na mama yangu mzazi,” alitiririka Diamond.
TURUDI KWA MZEE ABDUL TENA
Baada ya kutoa maneno hayo makali kwa
mzazi wake huyo, Ijumaa lilizungumza na mzee Abdul ambapo alisema kwa
kifupi bila kufafanua: “Basi sawa siyo mwanangu.”
AKUMBUSHWA YA KANUMBA
Kwa mujibu wa mashabiki wa staa huyo mkubwa
wa Bongo Fleva waliozungumza na Ijumaa juu ya sakata lake na baba huyo
walimtahadharisha kwa kumkumbusha hali ilivyokuwa kwa marehemu Steven
Charles
Kanumba ‘The Great’ na baba yake mzee Charles Kusekwa.
“Platnumz
anatakiwa amalize suala hili kwa sababu nafikiri anakumbuka malumbano
ya Kanumba na baba yake ambayo hayakuwa mazuri,” alisema Luda wa
Kinondoni, shabiki namba moja wa Diamond.
TUJIKUMBUSHE
Wiki mbili zilizopita, mzee Abdul aliibuka na
kuliambia gazeti ndugu la hili, Amani, kuwa Diamond ni mwanaye lakini
hamjali na badala yake amekuwa akiponda starehe.
BADO UTATA
Hata hivyo, wiki moja baadaye ndugu wa Diamond
waliibuka na kudai kuwa mzee Abdul siyo baba halisi wa msanii huyo bali
baba halisi ni Idd Salum, ambaye alifariki mwaka 2004 ambapo Platnumz
hakufafanua suala hilo.
No comments:
Post a Comment