tangazo

Tuesday, July 10, 2012

MWENYEKITI WA MADACTARI AHOJIWA POLISI

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana lilimhoji Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi kuhusu kukaidi amri ya Mahakama iliyotaka wasitishe mgomo.
Juni 22, mwaka huu, Jaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha  Kazi, Sekela Moshi alitoa amri ya kusitisha mgomo huo akisema: “Kwa maelezo hayo, ninasitisha mgomo huo ulioitishwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), hivyo MAT na wanachama wake hawapaswi kushiriki mgomo huo kama walivyopanga hadi pande zote mbili zitakaposikilizwa.”

Katibu Mkuu wa MAT, Dk Edwin Chitega alikaririwa na vyombo vya habari akisema akisema: “Mgomo wetu hauwezi kuzuiwa na Mahakama, utazuiwa kwa madai yetu kutekelezwa.”
Polisi kanda hiyo maalumu ya Dar es Salaam, ilithibitisha kumhoji Dk Mkopi jana na Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Ahmed Msangi alisema kiongozi huyo alifika Kituo cha Kati cha Polisi kuhojiwa na kisha aliondoka.

“Ni kweli amekuja mwenyewe. Tumechukua maelezo yake na ameshaondoka,” alisema Msangi.
Akizungumzia suala hilo, Chitage alisema mwenyekiti wake alitumiwa taarifa ya kutakiwa katika Kituo hicho cha Polisi Kati kwa simu kutoa maelezo juu ya madai ya kukaidi kutekeleza amri ya Mahakama iliyotolewa Juni 22, mwaka huu ikiitaka MAT kusitisha mgomo ulioanza Juni 23, mwaka huu nchini kote... “Alinipigia simu na kunieleza kuwa yupo huko tangu saa 5.00 asubuhi.”

Amri ya Mahakama
Mahakama hiyo ilitoa amri kuwataka madaktari hao kuendelea na kazi hadi madai yao ya msingi katika mgogoro huo yatakaposikilizwa.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Moshi alisema zuio hilo ni la muda na linalenga kupata fursa ya kusikiliza kwanza maombi ya msingi kuhusu mgogoro huo.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa bila wawakilishi wa MAT, Jaji Moshi alipanga siku ya kusikiliza maombi hayo ya msingi na kueleza kuwa hukumu itakayotolewa, itafungua ukurasa mpya kuhusu mgogoro huo.

Mapema kabla ya amri hiyo ya Mahakama kutolewa, madaktari walisisitiza kutekeleza azma yao ya kugoma kwa kubandika matangazo ya kuhamasishana kwenye kuta za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi).

MAT waomba ulinzi UN

Katika hatua nyingine, MAT imetoa tamko jipya jana ikiomba Umoja wa Mataifa(UN), kumwekea ulinzi Dk Steven Ulimboka katika hospitali aliyoko baada ya taarifa kueleza kuwa kuna timu ya wauaji imetua nchini Afrika Kusini kuhakikisha harudi nyumbani akiwa hai.
Tamko hilo lilitolewa jana na Dk Mkopi ambaye aliomba pia UN iwawekee ulinzi wadau wote wanaohusika katika masuala hayo.

“Tunataka pia, Mahakama ishauriwe kuacha kutumiwa kwa faida ya siasa na Bunge libaki na kazi ya kuhakikisha linaisimamia Serikali kutokana na vifo na mateso wanayopata watu kutokana na mgomo unaoendelea,” alisema Dk Mkopi.

Hata hivyo, alisema wanakaribisha mawazo kutoka kwa mashirika ya kimataifa ya jinsi gani wanaweza kutatua tatizo lililopo.

Wizara yakata posho

Wakati huohuo; Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesitisha posho za madaktari waliokuwa mafunzoni ambao wamegoma hadi hapo itakapopata taarifa ya uchunguzi wa Baraza la Madaktari.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo jana na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, Regina Kikuli ilisema posho za madaktari hao waliogoma zimesitishwa rasmi kuanzia Julai Mosi, mwaka huu hadi uchunguzi wa Baraza la Madaktari utakapokamilika.

Taarifa hiyo ilisema wizara hiyo ilipokea malalamiko kuwa kati ya Juni 23 hadi Juni 29, mwaka huu madaktari 372 walio katika mafunzo kwa vitendo kati ya 763 katika hospitali mbalimbali nchini, waligoma kutoa huduma kwa wagonjwa kinyume cha wajibu wao.

Ilisema kitendo hicho siyo tu kilihatarisha usalama wa wagonjwa waliohitaji huduma za matibabu katika hospitali hizo, bali kilikuwa ni ukiukwaji wa maadili ya taaluma.

Sehemu ya taarifa hiyo iliongeza kwamba, hivi sasa madaktari hao hawako maeneo yao ya kazi na suala hilo limepelekwa Baraza la Madaktari kwa uchunguzi kuhusu kitendo walichokifanya.

“Kwa kuwa wizara ndiyo yenye dhamana ya usimamizi wa huduma za afya nchini na kwa kuwa madaktari hao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika, hivyo wizara imewasilisha malalamiko haya huko ili liwachunguze na kuamua hatima yao kitaaluma,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:
“Wizara inasitisha posho zao kuanzia Julai Mosi, 2012 hadi hapo itakapopata taarifa ya uchunguzi wa Baraza la Madaktari.”

Kuhusu madaktari wengine waliogoma, taarifa hiyo ilisema   taratibu za kiutumishi zitachukuliwa na mamlaka ya ajira zao kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

Madaktari hao waliokuwa katika mafunzo ya vitendo waliogoma, walirejeshwa wizarani kwa barua kutoka kwenye mamlaka za hospitali walikokuwa wakifanyia mafunzo kwa vitendo.
Wakati wizara ikisimamisha posho za madaktari hao waliokuwa mafunzoni kwa kugoma kutoa huduma, Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imesema kuwa, huduma za afya hospitalini hapo zimerejea katika hali ya kawaida.

Taarifa ya bodi hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Profesa Joseph Kuzilwa iliyotolewa jana kwa umma ilisema kwa mujibu wa tathmini yake iliyofanyika Julai 7, mwaka huu madaktari wote waliorejea kazini wanaendelea na kazi kama kawaida.

No comments:

Translate