tangazo

Tuesday, July 10, 2012

DR SLAA. LEMA,MNYIKA MATATANI

                                                 Katibu Mkuu wa Chadema,Dk Willibrod Slaa

POLISI KUWAHOJI KWA MATAMSHI KWAMBA WANATISHIWA MAISHA, DK NCHIMBI ASEMA WANASABABISHA CHUKI




KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema huenda wakajikuta matatani kutokana na madai waliyoyatoa juzi kwamba wanatishiwa kuuawa na kigogo mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa.Kutokana na matamshi hayo, jana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi ameliagiza Jeshi la Polisi kuwahoji viongozi hao ambao walidai kuwa mauaji hayo yamepangwa kufanywa kwa kuwekewa sumu kwenye chakula au kwa kutumiwa makundi ya ujambazi.

Akizungumza na waandishi wa mjini hapa jana, Dk Nchimbi alisema licha ya kudai kwamba wanatishiwa, ameshangazwa na msimamo wa viongozi hao kukataa kupeleka suala hilo polisi kwa madai ya kuhofia suala hilo halitafanyiwa kazi.

Alisema watawahoji viongozi hao kwa sababu suala la usalama wa Mtanzania yeyote si la hiari, bali ni la kikatiba na la kisheria hivyo, ni lazima polisi watimize wajibu wao.

“Ni lazima tuwahoji ili tujue ni nani amewatisha na kwa sababu zipi. Hatutamuomba mtu ruhusa ya kumlinda kwa sababu huo ni wajibu na kazi yetu kuwalinda raia, hilo halina mjadala. Hatua zitachukuliwa endapo itabainika kuwa madai yao yana ukweli,” alisema Dk Nchimbi.

Aliwataka viongozi  wote wa kisiasa wakiwamo wa Chadema wanapohisi kutishiwa usalama wao, watoe taarifa polisi ili vyombo vya dola viyafanyie uchunguzi malalamiko yao ili utaratibu ufanyike kuhusu usalama wao kama sheria inavyotaka.

Alionya tabia ya viongozi kuzungumza nje ya utaratibu akisema haikubaliki kwani inaweza kuwa ni mbinu za kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Dk Nchimbi alisema jambo hilo si jema kwani linajenga hofu miongoni mwa Watanzania na kuwafanya wasiviamini vyombo vyao vinavyowalinda kwa mujibu wa sheria.
“Ni kweli kuwa kila mwanasiasa anataka kukubalika na umma lakini, akubalike katika taratibu zinazokubalika,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:

“Ingekuwa Serikali inataka kukubali umaarufu kama huo, basi ingetumia mwanya wa haohao Chadema wakati mitandao ya kijamii iliposambaza taarifa kuwa Chadema ilihusika na kifo cha marehemu, Chacha Wangwe.”

Alisema Serikali haikukurupuka na kuwakamata, badala yake ilifanya uchunguzi kwanza na matokeo yake alikamatwa  dereva wake ambaye ameshachukuliwa hatua.
Alisema kama Serikali ingekuwa inatafuta umaarufu, ilikuwa ni fursa nzuri kwake kujipatia umaarufu na kukivuruga chama hicho kwa kuwakamata viongozi wa Chadema hasa baada ya kuwapo kwa uvumi kwamba wamemuua kiongozi huyo.

“Viongozi wetu wa kisiasa ni lazima wafanye mambo ambayo kesho na keshokutwa watakiri mchango wao, ama katika ujenzi au uharibifu wa nchi yetu. Kila siku wakilalamika kuwa wanataka kuuawa basi ni lazima watu watawashangaa kwani badala ya kutatua matatizo ya wananchi wanabaki wakilalama wanataka kuuawa. Watu kama hawa wanafanya hivi kwa masilahi yao, wanaweza kuwagombanisha wananchi.”

Waziri Nchimbi aliwataka wananchi na viongozi wa kisiasa kuondoa hofu kwani Serikali ina wajibu wa kuwalinda na hakuna mtu atakayenufaika kwa mauaji ya wanasiasa hao.

Kuhusu madai kwamba polisi wamekuwa wakipuuza malalamiko ya wapinzani, Dk Nchimbi alikiri kuwapo kwa baadhi ya polisi wenye kasoro katika utendaji wao lakini akasema wengi ni waadilifu.
Alisema ikiwa kuna mtu haridhishwi na utendaji wa polisi kwa kutopata huduma kama inavyostahili, ana uhuru wa kutoa taarifa katika ngazi za juu hata ikiwa ni kwake.

Ikulu nayo yatoa tamko

Katika hatua nyingine, Ikulu imesema hakuna mpango wowote unaoratibiwa na Idara ya Usalama wa Taifa kwa lengo la kuwaua viongozi hao wa Chadema.
Jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alihoji sababu za Serikali kutaka kuwaua viongozi hao wakati si tishio lolote kwa nchi.

Balozi Sefue alisema Idara ya Usalama wa Taifa haiko kwa ajili ya kuua raia au viongozi, bali kulinda masilahi ya taifa na kuhoji: “Sasa kwa nini wauawe? Wana nini hasa hadi Idara ya Usalama ifanye hivyo?”

Alisema ni vyema wakati mwingine kukawa na umakini kwa kuangalia namna siasa zinavyoweza kufanya kazi... “Hii inaweza kuwa siasa tu. Sisi serikalini hatuna mambo ya vyama, tunafanya kazi kwa ajili ya watu wote.”

Alisema Idara ya Usalama wa Taifa na Serikali hazifanyi kazi kisiasa, bali kwa kuangalia masilahi ya Watanzania wote: “Huku serikalini sisi hatuna ugomvi na wanasiasa. Tunafanya kazi na watu wote.”
Alisema wanaoweza kufikiria kuwa kuna siasa katika Serikali na vyombo vyake wao ndiyo wanaweza wakawa wanafanya siasa.

Tuhuma za Chadema
Kauli hizo za Serikali zinatokana na tuhuma za Chadema kwamba kimebaini njama za kuwaua viongozi wake hao waandamizi ambazo zinaratibiwa na kigogo mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba nyendo zao zimekuwa zikifuatiliwa kwa saa 24.

Tuhuma hizo za Chadema zilitolewa juzi na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni akisema: “Sisi Chadema hatuna mambo ya siri tunayotaka kufanya katika nchi hii. Matatizo ya Watanzania yapo wazi na yanajulikana na kila mmoja, Serikali ya CCM itekeleze sera na ahadi zao kwa wananchi na si vitisho.”

No comments:

Translate