Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI)
kushoto ni Azzan Khalid Hamdan, Msellem Ali Msellem, Farid Hadi Ahmed,
Khamis, na Mussa Juma Issa wakiswali katika Msikiti wa Mbuyuni kabla ya
kusambaratishwa na Kikosi cha kutuliza Ghasia (FFU)
JESHI la Polisi Nchini, linawatafuta viongozi wa Taasisi za kidini na
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar (Jumiki) huku
likiwashikilia watu 43 wanaodaiwa kuhusika na vurugu zilizotokea
juzi. Viongozi wanaotafutwa na Jeshi la Polisi na ambao wanatakiwa
kujisalimisha ni pamoja na Msemaji wa Taasisi za Kidini, Farid Hadi
Ahmed, Kiongozi wa Uamsho, Mselem Ali Mselem, Naibu Kiongozi wa Uamsho,
Azan Khalid Hamdan na na Mhadhiri wa Uamsho Mussa Juma Issa.
Lakini Naibu Kiongozi wa Uamsho, Hamdan alikanusha jumuiya yake kuhusika
na vurugu hizo akisema walikuwa msikitini kuwaombea dua waliofikwa na
maafa katika meli ya MV Skaget Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini
Magharibi, Azizi Juma Mohamed alisema jana kuwa viongozi hao wanatafutwa
kwa kosa la kuwahamasisha vijana kufanya vurugu na kusababisha
uharibifu wa miundombinu.
Alisema katika vurugu hizo, vijana hao walikata miti iliyomo pembeni mwa
barabara, kuvunja vioo vya nyumba na magari , kuweka mawe na vitu
vizito barabarani. Kamanda alisema viongozi hao waliomba kibali cha
kufanya mikutano kwenye uwanja wa mzalendo ili kuwaombea dua waliokufa
kwa ajali ya meli ya Mv Skagit lakini polisi ilikataa kutokana na amri
ya serikali kuzuia mihadhara.
Kamanda Azizi alisema kwa kuwa kundi hilo la Uamsho linafahamika kwa
ubishi ndipo jeshi hilo lilipeleka polisi kwenye uwanja wa Mzalendo ili
kuzuia mkusanyiko wa wafuasi hao wa Umsho.
“Polisi waliwahi kuwazuia wafuasi hao wasikusanyike kwenye viwanja hivyo
lakini viongozi wa Uamsho waliwatangazia wafuasi wao wakiwataka sasa
wakusanyike kwenye viwanja vya msikiti wa Mbuyuni karibu na eneo la
Malindi,” alisema Kamanda.
Alisema muda wa kuomba dua ulipofika viongozi hao waliingia msikitini lakini watu wengi zaidi walikuwa nje ya msikiti huo.
Kamanda alisema kilichoendelea kwenye msikiti huo ni viongozi huo ni kwa
viongozi hao kukashfu viongozi wa serikali na kuwataka wafuasi wao
kutounga mkono muungano.
Alisema wakati hayo wakiendelea,wafuasi wa Uamsho wakiwa na bendera
walianza vurugu kupanga mawe barabarani na kuchoma moto matairi. Alisema
ndipo Jeshi la Polisi likaamua kutumia nguvu kuwatawanya kwa mabomu ya
machozi na maji yenye kemikali za kuwasha.
Akijibu tuhuma hizo, Naibu Kiongozi huyo wa Uamsho, Hamdan vurugu hizo
zimesababishwa na polisi wenyewe kwani wao walikuwa msikitini wakiomba
dua waliofikwa na maafa ya ajali ya Mv Skaget.
“ Tunasikitika sana viongozi wa dini kuhusishwa na vurugu zilizotokea
jana (juzi), kwa kweli sisi hatuhusiki na vurugu hizo na tumeshangazwa
na Jeshi la Polisi kuvamia msikitini na kuanza kuwatawanya waumini
waliokuwa wakifanya ibada,” alisema.
Alisema baada ya sala hiyo walitoa mawaidha ya kuwataka waumini wao
wasiilaumu serikali katika tukio la ajali na wachukulie kwamba huo ni
mtihani kutoka kwa Mungu. Hamdani alisema hata kama vijana hao walibeba
bendera za Uamsho wao lakini hawana uhusiano wowote na jumuiya yao.
“Bendera ni kitambaa ambacho mtu yoyote anaweza kuwa nacho na
isichukuliwe kila mwenye bendera ya Uamsho ni mwanachama wa jumuiya
hiyo,” alisema
Alishangazwa na Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa kwa kurusha mabomu
hadi mitaani hasa katika kipindi hiki ambacho watanzania wanaomboleza
vifo vya ndugu na jamaa zao waliopotea katika ajali ya meli.
No comments:
Post a Comment