tangazo

Tuesday, July 10, 2012

Migiro akwepa kuzungumzia urais



 ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk Asha-Rose Migiro ambaye amerejea nchini jana alikwepa kuzungumzia suala la kuwania urais, huku akisisitiza kuwa kwa miaka kadhaa atakuwa nje ya ulingo wa siasa.

Dk Migiro ambaye aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 9:30 alasiri, alipoulizwa kama ana mpango wa kuwania urais mwaka 2015, alishindwa kukubali wala kukataa na badala yake alisema atajikita zaidi katika taaluma yake ya ualimu.

Kauli ya Dk Migiro imekuja kipindi ambacho jina lake limekuwa likitajwa katika nafasi ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete, atakapomaliza muda wa uongozi wake hapo mwaka 2015. Kabla ya kwenda UN alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Dk Migiro ambaye mwaka 2007 aliteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-Moon kushika wadhifa huo, alisema anafurahi kumaliza miaka mitano kwa mafanikio, kwamba ataripoti Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Kitivo cha Sheria kwa kuwa wakati anaondoka alichukua likizo isiyo na malipo ambayo imemalizika mwishoni mwa mwaka jana.

Juzi, Dk Migiro alitoa waraka maalumu akisema kwamba mwisho wa utumishi wake katika umoja huo ni mwanzo utekelezaji wa majukumu mengine hapa nchini.

Katika waraka huo ambao Mwananchi lilifanikiwa kupata nakala yake , Dk Migiro alisema, "Hakika, kila chenye mwanzo hakikosi mwisho na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa jingine."

Lakini, jana baada ya kuwasili nchini na kupokewa na watu mbalimbali akiwamo Waziri wa Mmabo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe, alizungumza na waandishi wa habari  na kueleza mambo mbalimbali likiwamo suala la kama atagombea  urais 2015, kama atajitosa kuwania  nafasi yoyote ndani ya CCM.

Urais 2015
Akizungumzia suala la urais alisema, “Kwa taarifa tu ni kwamba nchi hii tayari inaye Rais na mimi baada ya kumaliza kipindi changu cha miaka mitano UN nina hamu ya kurejea nchini”,

 “Nimerejea kama mama wa familia, kama dada na kama mwalimu.”

Alisema kuwa wakati anaondoka nchini alikuwa mwajiriwa wa UDSM na kwamba alichukua likizo isiyo na malipo ambayo imemalizika mwishoni mwa mwaka jana.

“Kama mnavyowaona wahadhiri (mabosi) wangu wa Chuo Kikuu wamekuja kunipokea na mimi nikifika tu nitatoa taarifa katika Kitivo cha sheria na Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu ch Dar es Salaam,” alisema Dk Migiro.

Alisema kutokana na taratibu za UN zilivyo ni vigumu mtu kumaliza muda wake na wakati huo huo akajiingiza katika majukumu mengine kama siasa, kwa kuwa akikutwa na jambo lolote bado atatolewa mfano kama mtu aliyewahi kushika nafasi ya juu ndani ya umoja huo.

“Nitakuwa nje ya siasa kwa kipindi fulani…, ukimaliza muda wako UN kuna taratibu ambazo unatakiwa kuzifuata na kuzizingatia, pia siku mbili kabla ya kumaliza muda wangu Ban Ki-Moon aliniteua kuwa mjumbe wa Kamati ya Ukimwi hivyo pia sijajua majukumu yangu yatakuwaje” alisema Dk Migiro.

Dk Migiro pia alipongeza suala zima la kuanza kwa  mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya, kufafanua kwamba ndani ya umoja huo moja ya mambo aliyokuwa akiyasimamia ni suala zima na utawala wa sheria na haki za binadamu na kuongeza kuwa nchi kuwa na Katiba mpya ni jambo la msingi.

“Mambo mengi ya msingi yatabebwa ndani ya Katiba Mpya, naona faraja sana Tanzania kujiunga na nchi nyingine ambazo zimeimarisha Katiba zao” alisema Dk Migiro.

Dk Migiro ambaye jana ilikuwa siku yake ya kuzaliwa, pia aligusia changamoto alizokutana nazo wakati akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo ikiwa ni pamoja na nchi nyingi kuwa masikini, huku akisisitiza kwamba kwa sasa umepungua na nchi hizo kupiga hatua katika suala zima la usalama wa chakula baada ya kujiwekea Malengo ya Milenia (MDG’S).

No comments:

Translate