Marehemu Banzi
Jeneza lenye mwili wa Marehemu Banzi
Baadhi ya waombolezaji wakiwa katika Msiba wa marehemu Banzi.
Marehemu Fikiri
Marehemu Hekima Bakari
Marehemu Mohamed Bakari
UKWELI
kamili kuhusu vifo vya watu sita waliokunywa gongo Kigogo Sambusa
Luhanga Darajani, ambapo wengine wamelazwa wakiwa hoi katika Hospitali
ya Amana jijini Dar es Salaam umebainika.
Gazeti hili limegundua
kuwa gongo waliyokunywa ilikuwa ina mchanganyiko wa kemikali mbalimbali
na dawa za viwandani na tayari sampuli yake imepelekwa kwa mkemia mkuu
wa serikali kwa uchunguzi zaidi.
Mteja mmoja ambaye kwa kipindi cha
nyuma alikuwa ‘mnywaji mzuri’ wa gongo katika eneo hilo ambaye hakutaka
atajwe gazetini alichambua jinsi pombe hiyo inavyotengenezwa.
Alisema kuwa kuna kemikali zinozotumika kutengezea konyagi ambapo
watengenezaji wanazipata katika kiwanda kimoja (jina tunahifadhi) na
wanachanganya na dawa nyingine.
Alibainisha kuwa kemikali moja
hujazwa kwenye chupa ya ujazo wa lita moja na kuchanganywa na maji kiasi
cha lita kumi kisha hutiwa spiriti pamoja na dawa ya madoa iitwayo
‘jick’ na mchanganyiko huo huzalisha kitu kinachoitwa gongo na kuanza
kusambaziwa wateja.
Chanzo hicho kilisema kuwa njia hiyo ndiyo
aliyokuwa akiitumia Hekima Bakari kwa muda mrefu, mama anayedaiwa
kuwauzia gongo watu waliofariki na kulazwa Hospitali ya Amana.
Kiliendelelea kufafanua kuwa mama huyo ametengeneza mtandao na alikuwa
akisambaza kinywaji hicho Gongo la Mboto, Kipunguni, Chanika, Kitunda,
Kimara Bucha na Kigamboni.
Gongo hiyo ilianza kuua Jumatatu ya wiki
iliyopita ambapo ilimuua Juma Abdallah baada ya kunywa kinywaji hicho na
wanywaji wengine wakawa wanajificha kwa kuwa walikuwa wakiogopa
kukamatwa na polisi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya mtaa
katika eneo hilo la Kigogo Mbuyuni, Mohammed Mnunga aliwataka wote
waliokunywa gongo hiyo kujitokeza na kwenda kupimwa afya zao kwa usalama
wao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Charles
Kenyela amepiga marufuku mtu yeyote kujihusisha na kupika, kuuza au
kunywa pombe haramu ya gongo na akasema tayari watu kadhaa wamekamatwa
kuhusiana na sakata hilo.
Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa hadi
sasa kuwa ni Ramadhan Selestin (30), Salehe Omary (17), Shukuru Marungu
(20), Charles Ibrahim (20), Fadhili Juma (20) wote ni wakazi wa Kigogo
na Abdallah Mnazi (30) mkazi wa Tabata.
Aliwataja pia waliofariki
katika nyakati tofauti kuanzia Julai 7 hadi 12, mwaka huu, katika maeneo
ya Kigogo Mbuyuni kuwa ni Juma Abdallah (60), Mathew Roman (35), Khalid
Hamis (31), Mohamed Said (25) na Antipal Raphel (60) wote wa Kigogo
Mbuyuni na Hekima Bakari, ambaye ni muuzaji wa gongo hiyo.
No comments:
Post a Comment