Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia Julai
19 hadi Julai 21 kufuatia maafa ya ajali ya Meli ya Mv. Skagit iliyozama karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein
akitangaza maombolezo hayo, alisema bendera zote zitapepea nusu
mlingoti na kwamba shughuli za sherehe na burudani zimefutwa kwa muda wa
siku tatu za maombolezo.
Dk.
Shein alisema shughuli za Serikali zitaendelea kama kawaida. Katika
taarifa yake aliyoitoa Ikulu usiku wa kuamkia Julai 19, Rais Dk Shein
amewahakikishia wananchi na hasa waliopoteza jamaa zao kuwa Serikali
itabeba gharama zote za mazishi na pia kugharamia huduma za matibabu kwa
majeruhi.
“Nimesikitishwa sana na msiba huu,
Katika wakati huu si vema tukaanza kulaumiana jambo la muhimu hivi sasa
ni kuokoa maisha ya watu” Alisema Rais Dk. Shein.
Mbali
ya taarifa hiyo, Rais Dk Shein aliungana na wananchi, viongozi wa
Serikali, vyama vya siasa, Viongozi wa dini katika kutambua maiti
zilizofikishwa katika eneo maalum la viwanja vya Maisara Suleiman.
Mbali
ya kwenda katika viwanja hivyo, pia alifika katika eneo la bandari ya
Zanzibar kufuatilia taarifa za tukio hilo. Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania jana lilisitisha shughuli zake kufuatia maafa hayo ambapo
wakati wa jioni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi
alitarajiwa kufanya majumuisho ya bajeti yake.
Baadhi
ya Wabunge wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa,Shamsi Vuai Nahodha, Mkuu wa Jeshi la Polisi walitembelea majeruhi
katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na eneo la viwanja vya
Maisara ambapo maiti hufikishwa kwa ajili ya utambuzi.
Mbali
ya Bunge, pia Baraza la Wawakilishi Zanzibar jana lilisitisha kwa muda
shughuli zake ili kutoa nafasi kwa Wawakilishi hao wa wananchi kushiriki
katika shughuli za uokozi ambapo wengi walifika bandarini kusaidia kazi mbalimbali ikiwemo kuwafariji waliopoteza ndugu zao.
Taarifa
kutoka Mamlaka za Serikali zinaeleza kwamba hadi asubuhi hii maiti 30
zilipatikana ambapo 20 kati ya hizo zimetambuliwa na kuchukuwa na jamaa
zao huku wananchi wengine wakiendelea na kuzitambua maiti zinazofikishwa
katika eneo la Maisara.
Aidha,
katika taarifa hiyo, watu 145 wameokolewa wakiwa hai, wengi wao wapo
katika hali nzuri wameruhusiwa kuungana na familia zao baada ya kupatiwa
matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Zanzibar.
Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai
18,2012 saa 7:50 mchana ikitokea Bandari ya Dar es Salaam kwenda
Zanzibar ikiwa imebeba abiria 250 watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6.
Kazi ya utafutaji na uokoaji
zinaendelea asubuhi hii katika eneo la tukio ilikozama meli hiyo umbali
wa maili sita Kusini mwa Kisiwa cha Yasin karibu na Kisiwa cha Chumbe
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment