TAMASHA la Majahazi, ZIFF linalofanyika kila mwaka limeanza juzi kwa
staili ya aina yake kwa mashindano ya Ngalawa kutoka Forodhani mpaka
fukwe za Chukwani visiwani Zanzibar.
Ngalawa hizo zilipewa majina
ya baadhi ya kampuni zinazodhamini tamasha hilo na Zanlink wanaotoa
huduma ya mtandao ndiyo waliibuka washindi na kunyakua kiasi cha Sh
200,000.
Mshindi wa pili ilikuwa ni kampuni ya Zat iliyopata Sh
150,000 na Mtoni Marine ilishika nafasi ya tatu na kupata kiasi cha Sh
100,000.
Akizindua tamasha hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa ZIFF,
Ikaweba Bunting alisema tamasha la mwaka huu kama yaliyopita
limemejikita katika kuleta burudani, kuwaunganisha watu wa tamaduni
mbalimbali, kutoa ajira kwa Watanzania hasa vijana na kuchangia katika
pato la taifa.
“ZIFF ni kiungo muhimu katika kubadilishana
utamaduni, kuanzia leo watu kutoka nchi mbalimbali wanakutana, tunaleta
siku tisa za kubadilishana utamaduni na kujifunza, Watanzania itumieni
fursa hii kujifunza na pia kuonyesha taswira nzuri ya taifa letu,”
alisema Bunting na kuongeza;
“Tunaomba muendelee kutuunga mkono kwa kuwa kila mwaka wakati wa tamasha
tunaajiri vijana wapatao mia nne, haya ni mafanikio makubwa kwetu na
kwa taifa kwa ujumla,” alisema Bunting.
Tamasha la ZIFF
litaendelea kwa siku tisa mpaka Julai 15, ambapo mbali na kuonyesha
filamu pia litakuwa likisindikizwa na burudani za muziki kutoka kwa
wanamuziki nyota wa ndani na nje ya Tanzania.
Nyota
watakaolipamba tamasha mwaka huu ni pamoja Jose Chameleone (Uganda),
Diamond, Linah, Barnaba, Roma, THT, Dossar, Tausi Women Group,Tazneem.
Upande
wa filamu mwigizaji kutoka Marekani, Mario Van Peebles atakuwa mgeni
mashuhuri wa mwaka huu na anatarajiwa kuzindua filamu yake, 'We The
Party' katika ukumbi wa Cinema Century uliopo mlimani City jijini Dar es
Salaam.
Wasanii wa filamu watakaohudhuria ni pamoja na Irene
Uwoya, Jackline Wolper, Issa Musa, Jacob Steven, Steve Nyerere na
wengine wengi.
No comments:
Post a Comment